MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kuwa mvua zilizoanza kunyesha nchini ni endelevu, huku wananchi wakitakiwa kufuatilia taarifa za utabiri unaotolewa.
Hali hiyo inakuja baada ya TMA kutoa utabiri Oktoba mwaka huu, kueleza kuwa jua la utosi limeingia nchini, hali iliyosababisha kuongezeka kwa joto, huku mikoa ya Dar es es Salaam, Kilimanjaro na Ruvuma ikirekodi kiwango cha juu cha joto na kuongezeka kwa ukame uliosababisha mifugo na wanyama kufa.
Katika utabiri huo TMA ilisema kuwa kutakuwa na kipindi cha ukame huku mvua zikitarajiwa kuanza kunyesha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi huu.
Kwa sasa mvua zinanyesha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Mwanza na Rukwa.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri cha TMA, Samuel Mbuya, alisema mvua zilizoanza kunyesha zilizotabiriwa kwenye utabiri wa TMA wa Oktoba mwaka huu.
"Hizi ni mvua zile ambazo tulizitabiri, na zimeanza sasa kunyesha, kikubwa tunawaomba wananchi na wadau wote kufuatilia utabiri wetu wa kila saa na kila siku ambao tunautoa kila siku," alisema Mbuya.
Aidha, alisema mvua hizo zinatarajia kuendelea kama ambavyo walitabiri.
"Bado hakuna mabadiliko makubwa, tunatarajia mvua zitaendelea kusambaa kwenye maeneo mbalimbali, TMA tutaendelea kutoa taarifa ili wananchi wafahamu na kuchukua tahadhari," alisema Mbuya.
Kutokana na kuongezeka kwa ukame viongozi mbalimbali wa dini wamefanya ibada ya kuomba mvua, huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), likitangaza kupungua kwa uzalishaji wa umeme kwa megawati 345 sawa na asilimia 21 kwenye vituo vyake vitatu vya Kihansi, Kidatu na Pangani.
Aidha, katika baadhi ya maeneo kuna mgawo wa umeme, huku wengine wakilazimika kutumia majenereta kupata nishati, na TANESCO ilieleza kuwa inaelekeza nguvu kwenye umeme wa gesi ili kuzalisha megawati 358.
Pia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ilitangaza ratiba ya mgawo wa maji maeneo mbalimbali kutokana na kupungua kiasi cha maji Mto Ruvu, huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiagiza kuchukuliwa maji ya bwawa la asili ili kuongeza kiasi cha maji kwenye mto huo.
Hatua nyingine ni kupiga marufuku shughuli za kilimo na kupepusha maji Mto Ruvu.
Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni aliziagiza kamati za ulinzi na usalama kusimamia na kulinda vyanzo vya maji dhidi ya uharibifu, ambao umechangia ukame.