Mapingamizi yalivyoighubika kesi ya kina Mbowe




Mahakama Kuu (Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi) imetupilia mbali mapingamizi manane kati ya tisa yaliyoibuliwa na mawakili wanaomtetea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uhujumu uchumi.


Idadi hiyo imeongezeka baada ya mahakama hiyo Jumatatu kutupilia mbali pingamizi ambapo mawakili wa utetezi walikuwa wanapinga mahakama isipokee Kitabu cha Kumbukumbu za Mahabusu cha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, cha mwaka 2020 ili kiwe kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri.



Jopo la mawakili hao linaloongozwa na Peter Kibatala lilipinga kitabu hicho kisipokewe kama kielelezo cha ushahidi wa shahidi wa pili katika kesi ndogo, askari mpelelezi Ricardo Msemwa.



Mawakili hao walidai hapakuwa na amri ya mahakama ya kukiondoa mahakamani kielelezo hicho kwa kuwa kilishapokewa mahakamani katika kesi ndogo iliyohusu uhalali wa maelezo ya mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa.



Pia walidai kuwa kielelezo hicho tayari kilishatolewa uamuzi katika kesi hiyo ndogo, na kwamba mahakama haiwezi kukizungumzia tena, kwa kuwa ilikwishakikataa.



Walidai pia upande wa mashtaka hauna mamlaka ya kukileta tena mahakamani kwa sababu mahakama ilikwishakitolea uamuzi.



Mbowe na wenzake -- Halfan Bwire Hassa, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya wanakabiliwa makosa ya kupanga kutekeleza na kufadhili ugaidi.



Mapingamizi tisa

Tangu kesi hiyo ilipoanza katika hatua ya usikilizwaji wa awali Agosti 31, mwaka huu hadi jana, tayari mawakili wa utetezi walikuwa wameibua mapingamizi hayo tisa, huku yote yakitupiliwa mbali isipokuwa moja.



Utetezi waliibua pingamizi la kwanza Agosti 31 walipopinga mamlaka ya mahakama hiyo katika kusikiliza kesi ya ugaidi.



Mara tu ya kesi hiyo ilipoitwa, wakili Kibatala aliibuka na kudai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.



Alidai kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002, kesi hiyo ilipaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya kawaida na si divisheni hiyo, ambayo ni maalumu kwa kesi ya uhujumu uchumi.



Pingamizi hilo lilitupiliwa mbali na Jaji Elinaza Luvanda ambaye ndiye alikuwa jaji wa kwanza kusikiliza kesi hiyo. Jaji Luvanda alikubaliana na mawakili wa Serikali kuwa mahakama hiyo ndio yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.



Siku hiyohiyo mawakili hao walikuja na pingamizi lingine na kutaka mahakama iamuru washtakiwa waachiwe huru kwa madai kuwa Sheria ya Ugaidi iliyotumika kuwashtaki ina kasoro kutokana na kutokubainisha dhamira ya vitendo vya kigaidi.



Vilevile, walidai kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro za kisheria ambazo zilikuwa zinaifanya kesi hiyo kuwa batili.



Pingamizi hilo pia liligonga mwamba pale Jaji Luvanda alipolitupilia mbali, akieleza kuwa sheria hiyo iko sawa na kwamba kama wanadhani kuna kasoro basi wafuate utaratibu wa kuipinga.



Ingawa alikubaliana na sehemu moja ya hoja ya pingamizi, hiyo haikutosha kumaliza kesi hiyo. Badala yake aliuelekeza upande wa mashtaka kufanya marekebisho madogo kwenye hati ya mashtaka ili kutumia neno halisi lililotajwa kwenye sheria hiyo.



Pingamizi la tatu, wawakili wa utetezi walipinga maelezo ya mshtakiwa wa pili, Adam Kusekwa yasipokewe mahakamani kama kielelezo wakidai mshtakiwa huyo hakutoa maelezo hayo kwa hiyari.



Walidai aliteswa kabla na wakati wa kutoa maelezo hayo na kwamba yalichukuliwa nje ya muda uliowekwa kisheria.



Pingamizi hilo pia lilitupiliwa mbali na Jaji Mustapha Siyani alipewa jukumu la kusikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Luvanda kujiondoa kufuatia maombi ya washtakiwa waliodai kutokuwa na imani naye.



Jaji Siyani, pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa upande wa utetezi ulishindwa kuthibitisha mshtakiwa huyo aliteswa.



Katika pingamizi la nne, mawakili wa Mbowe waliiomba mahakama imwondoe shahidi wa sita, Mrajisi wa Leseni za Bunduki, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sebastiani Madembwe katika orodha ya mashahidi pamoja na ushahidi alioutoa.



Hoja yao ilikuwa kwamba maelezo yake hayakuwepo katika kitita cha maelezo ya mashahidi walichopewa washtakiwa, hivyo hayakuwa yamesomwa wakati wa kuhamishia kesi hiyo mahakamani kuu Kisutu na kwamba upande wa mashtaka haukuwa umeota maombi ya kumuongeza katika orodha ya mashahidi.



Hata hivyo, Jaji Joachim Tiganga ambaye amekuwa jaji wa tatu kusikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Siyani kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi, alilitupilia mbali.



Alikubaliana na hoja za Jamhuri kuwa kumbukumbu zinaonyesha kuwa maelezo yake yalisomwa na kwamba kilichotokea yalisahaulika tu kuwekwa kwenye kitita cha maelezo ya mashahidi walichopewa washtakiwa ila yalikuwemo kwenya jalada la mahakama.



Mawakili wa utetezi waliibua tena pingamizi la tano wakipinga upokeaji wa hati ya ukamataji mali kutoka kwa washtakiwa kwa madai kuwa ilikuwa imeandaliwa kwa sheria isiyokuwepo.



Jaji Tiganga alitupilia mbali hoja hizo akisema, pamoja na mambo mengine, kuwa upande wa utetezi wameshindwa kueleza namna gani wateja wao wameathirika kwa kunukuu sheria hiyo kimakosa, huku akirejea maamuzi ya Mahakama ya Rufani katika suala kama hilo.



Hivyo, alipokea hati hiyo iliyowasilishwa na shahidi wa nane, Mkuu wa Upelelezi, Wilaya (OC-CID) ya Arumeru mkoani Arusha, SSP Jumanne Malangahe na kuwa kielelezo cha ushahidi upande wa mashtaka.



Pingamizi la sita na pekee la utetezi kukubaliwa na mahakama likukuwa lile walilopinga kupokewa kwa Kitabu cha Kumbukumbu za Mahabusu katika kituo Kikuu cha Polisi (Central) Dar es Salaam, cha mwaka 2020 baada ya upande wa mashtaka kuomba kipokewe kwa ajili ya utambuzi.



Mawakili hao walidai, pamoja na mambo mengine kuwa, shahidi hakuweka msingi wala kuonyesha muunganiko wake na kitabu hicho.



Jaji Tiganga katika uamuzi wake alikubaliana na hoja za upande wa utetezi, hivyo akayakataa maombi ya Jamhuri kutaka kitabu hicho kipokewe.



Katika pingamizi la Saba, mawakili wa utetezi walipinga barua ya Naibu Msajili wa mahakama hiyo kwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), ambayo upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wa pili katika kesi ndogo (inayohusu maelezo ya Ling’wenya), askari mpelelezi, DC Ricardo Msemwa, walitaka ipokewe kwa utambuzi



Barua hiyo, ambayo pia ilimtaja shahidi huyo, ilikuwa ikijibu maombi ya kupatiwa Kitabu cha Kumbukumbu za Mahabusu cha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, ambacho kilishatolewa mahakamani hapo kama kielelezo cha upande wa mashtaka, katika kesi ndogo iliyohusu maelezo ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa.



Katika hoja zao walidai kuwa shahidi huyo hakuweza kueleza kuwa barua hiyo ilimfikiaje kwa kuwa hakuweza kuwasilisha Mahakamani kitabu cha kupokelea barua (dispatch book).



Hata hivyo, Jaji Tiganga katika uamuzi wake alitupilia mbali pingamizi hilo baada ya kukataa hoja za utetezi na akakubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa shahidi huyo alieleza kwa kiwango cha kuridhisha namna alivyoipata barua hiyo.



Katika pingamizi la nane mawakili wa utetezi waliiomba mahakama hiyo imuondoe shahidi huyo wa pili katika kesi hiyo ndogo pamoja na ushahidi wake kwa madai kuwa alipanda kizimbani na diary (shajara), simu na kalamau na kuvirejea wakati akitoa ushahidi wake kinyume cha sheria.



Jaji Tiganga katika uamuzi wake alitupilia mbali hoja hizo za utetezi, badala yake akaelekeza sehemu ya diary hiyo iliyokuwa na taarifa zilizohusu kesi hiyo zitolewe nakala na iwasilishwe mahakamani na upande wa utetezi ili wazitumie wakati wa kumhoji shahidi.



Pingamizi la Jumatatu linafanya jumla ya mapingamizi makubwa katika kesi hiyo kufikia tisa mbali na yale madogo madogo ambayo yamekuwa yakiibuliwa na mawakili wa utetezi kuhusiana na taratibu wakati mawakili wa Serikali wakiwaongoza mashahidi wao kutoa ushahidi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad