Wakati Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ikitoa taarifa ya kusitisha shughuli za utafutaji wa rubani Samweli Gibuyi, familia yake imedai kuonekana kwa kifaa cha kung’amua mwendo (Spidertracks) katika hema alilokuwa akiishi rubani huyo.
Taarifa hiyo ya TCAA iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi juzi ilieleza kuwa njia za utafutaji zimeshindwa kubaini alipo rubani huyo na ndege aliyokuwa inayomilikiwa na Pams Foundation, hivyo kinachofuata ni uchunguzi wa ajali kwa mujibu wa sheria.
Hayo yakijiri, mmoja wa ndugu wa rubani huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, aliliambia Mwananchi jana kuwa alipata taarifa ya kuonekana kwa Spidertrack kutoka kwa baba na kaka wa rubani huyo ambao baada ya kuona kifaa hicho walitoa taarifa kwa mamlaka husika, ikiwamo ofisi ya mkuu wa wilaya.
“Baba na kaka walinipa taarifa ya kukiona kifaa hicho Novemba 9 mwaka huu na kunitumia picha za kifaa hicho kupitia Whatsapp na nikawashauri kutoa taarifa kwa mamlaka husika na walifanya hivyo,” alisema.
Pia alieleza kuwa katika upekuzi uliofanywa awali katika hema alilokuwa akiishi rubani huyo kifaa hicho hakikuwa kimeonekana.
Meneja wa mradi wa Pams, Max Jenes alikiri kuwa na taarifa, akisema Spidertracks huwa zipo mbili, moja ikiwa ya akiba. “Bado tunafuatilia jambo hilo maana hata ndege hiyo iliporuka haikuonekana katika mifumo,” alisema.