Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, wamekamata na kuteketeza mashine 12 kati ya 35 zilizoingia nchini bila kufuata taratibu na sheria.
Akithibitisha kukamatwa kwa mashine hizo Wilayani Rombo, leo Jumamosi Novemba 6, 2021 Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema zimekamatwa baada ya malalamiko ya wazazi na walezi kudai maadili ya watoto wao yanaharibika kutokana na michezo ya Kamari inayochezeshwa kupitia mashine hizo feki.
Kamanda Maigwa amesema kufuatia malalamiko hayo kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Rombo pamoja na bodi inayosimamia mchezo huo kisheria waliendesha msako mkali na kukamata mashine 35.
" Mashine hizo zilizokamatwa 17 ni za bonanza, 5 za game show, 1 bet premier pamoja na feki 12 ambazo uchunguzi wake wa awali umebaini baadhi yake zimeingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi "amesema Maigwa
Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, James Mbarwe amesema bodi hiyo haitosita kuwachukukia hatua kali za kisheria kwa wanaokiuka taratibu za mchezo huo ikiwemo matumizi na uingizwaji kiholela mashine hizo