Mawakili wa kina Mbowe wamwekea pingamizi shahidi wa Jamhuri




 Mawakili wanaowatea Mwenyekiti wa Chedema na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi  wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi, wamemwekea pingamizi shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, wakiiomba Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iamuru sehemu ya ushahidi wake ambao ameshaanza kuutoa uondolewe kwenye kumbukumbu za mahakama.
Pingamizi hilo limetolewa na mawakili hao wa utetezi kupitia kwa wakili Jeremiah Mtobesya, muda mfupi baada ya shahidi huyo wa sita, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Sebastian Madembwe, kuanza kutoa ushahidi wake leo Alhamisi Novemba 4, 2021.

Wakili Mtobesya amieleza Mahakama kuwa maelezo ya shahidi huyo hayako kwenye mwenendo wa maelezo ya mashahidi yaliyotolewa Mahakama ya Kisutu.

Hivyo amedai kuwa kwa maana hiyo shahidi huyo anatoa ushahidi wake kinyume cha sheria na hivyo ushahidi wa shahidi huyo utakuwa haujaingia vizuri kwenye mwenendo na ameiomba mahakama itoe mwongozo.

Amedai kuwa upande wa mashtaka kama wakitaka kumtumia katika mazingira hayo walipaswa wawasilishe maombi rasmi chini ya kifungu cha 289 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), lakini hawajafanya hivyo.

"Pia tutaomba maelekezo kuhusu ushahidi wake ambao umeshaingia iwapo upande wa mashtaka watawasilisha maombi hayo na mahakama ikaridhia.", amehoji Wakili Mtobesya.

Hata hivyo Wakili Mtobesya amehoji iwapo itakuwa ni sahihi kuwasilisha maombi hayo kwa kuwa tayari shahidi ameshaanza kutoa ushahidi kabla ya Maombi kuwasilisha kwa mujibu wa Sheria.

Akijibu hoja za pingamizi hilo, kiongozi wa jopo la Waendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando ameiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pingamizi hilo akidai kuwa halina mashiko ya kisheria.

"Mheshimiwa Jaji pingamizi hilo halina mashiko youote kisheria. Kwanza limeletwa katikati ya ushahidi Ni kinyume cha utaratibu kabisa. Kama wangekuwa na hoja hiyo walitkiwa kuitoa mapema. Pengine ni matokeo ya kutokufuatilia mwenendo kwa umakini.", amedai wakili Kidando na kuongeza:

"Hoja yetu ya pili, Mheshimiwa Jaji ni kwamba shahidi huyu aliorodheshwa tangu kipindi cha committal proceeding (hatua ya usomaji wa maelezo ya mashahidi katika Mahakama ya Kisutu) katika rekodi za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ukrasa 32 Na jina lake ni namba 23."

Wakili Kidando amesema kuwa kiini cha ushahidi huo kilisomwa katika mwenendo wa shauri hilo katika mwenendo wa Agosti 23, 2020.

"Lakini pia katika ile orodha ya vielelezo nyaraka anayokuja kuizungumza (maelezo yake ya maandishi) imeorodheshwa namba 18 na imesainiwa naye shahidi, Sebastian Madembwe SSP.", ameongeza wakili Kidando na kusisitiza:

"Kwa hiyo katika hali yoyote ile hatukutakiwa kuleta maombi chini ya kifungu cha 289 CPA ili shahidi huyu aweze kutoa ushahidi wake

Pia Kanuni 8(2) ya Mahakama hii za mwaka 2016 takwa hilo la kisheria lilitekelezwa.

Hivyo Wakili Kidando amedai kuwa mbali na marekebisho madogo kwenye jina la shahidi hakuna kitu kipya ambacho wakili amekionesha na hivyo hakuna haja ya kuhoji uhalali wa ushahidi wake maana yuko hapa kihalali na ameomba pingamizi litupiliwe mbali na shahidi wao aweze kuendelea.

Kwa upande wake Mtobesya amedai kuwa upande wa mashtaka wamemshambulia kuwa hakuwepo tangu mwanzo, lakini akasema kuwa wanachokifanya ni kusaidia mahakama, hivyo kutokuwepo kwake tangu mwanzo hakuondoi uhalali wa hoja yake.

"Kwenye commital proceedings hakuna substance ya ushahidi wake. Substance Kuna vitu vitatu. Kwanza jina lake, hatukatai lipo lakini statement yake haipo, kuwa anakuja kusema nini. Statement hiyo ni ya muhimu sana.", amesisitiza Wakili Mtobesya na u mahakama itoe mwongozo kuhusu hilo.

Jaji Joachim Tiganga baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo kwa muda kwa ajili ya kuandika uamuzi.

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad