Milipuko ya Uganda :Mhubiri wa Kiislamu Anayehusishwa na Jihadi Auawa Kwa Kupigwa Risasi



Vikosi vya usalama nchini Uganda vimemuua kwa kumpiga risasi mhubiri wa Kiislamu anayetuhumiwa kufanya kazi na kundi la watu wenye silaha wanaohusishwa na milipuko ya kujitoa mhanga katika mji mkuu Kampala.

Maafisa walisema Sheikh Muhammad Abas Kirevu alikuwa amewaandikisha vijana kujiunga na seli za kigaidi zinazoendeshwa na Allied Democratic Forces (ADF) - waasi ambao wameahidi utiifu kwa kundi la Islamic State.


Takriban watu wanne waliuawa na washambuliaji waliokuwa kwenye pikipiki waliojilipua mjini humo siku ya Jumanne.


Zaidi ya wengine 30 walijeruhiwa katika shambulio hilo, ambalo IS ilisema ilihuika na maafisa wamelaumu ADF.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la ADF liliundwa nchini Uganda katika miaka ya 1990 lakini sasa lina makao yake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tangu kuahidi utiifu kwa IS mwaka 2019, Limezidi kufanya mashambulizi kwa jina la kundi hilo.

Watu 21 wamekamatwa tangu shambulizi la Jumanne, katika kile polisi wamekitaja kuwa ni kuvunjwa kwa seli za magaidi wa ADF mjini Kampala na kote nchini.

Msemaji wa polisi Fred Enanga alisema washukiwa 13 wakiwemo watoto kadhaa walinaswa walipokuwa wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia DR Congo.

Siku ya Jumatano, washukiwa wanne wa ADF waliuawa karibu na mpaka.

Msako pia unaendelea kumtafuta imamu mwingine, Sheikh Suleiman Nsubuga, ambaye anatuhumiwa kutoa mafunzo kwa magaidi, kuwapa mafunzo ya itikadi kali wanaoweza kusajiliwa na kutoa vifaa vya kutengenezea vilipuzi.

Shambulio la Jumanne lilikuwa la hivi punde zaidi katika milipuko kadhaa ya hivi majuzi ya bomu mjini Kampala.

Mwezi uliopita, mhudumu mwenye umri wa miaka 20 aliuawa baada ya kifaa, kilichoachwa kwenye begi la ununuzi, kulipuliwa kwenye baa moja jijini. Siku kadhaa baadaye watu kadhaa walijeruhiwa wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipojilipua ndani ya basi karibu na Kampala. Polisi wanasema wote wawili walihusishwa na ADF.

Mashambulio hayo ya Jumanne yaliashiria shambulio kubwa zaidi ambalo ADF imekuwa ikihusishwa nalo nchini Uganda tangu kuanzisha uhusiano na IS.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad