Mke Adaiwa Kumuua Mumewe na Kumfukia Kwenye Shimo la Kuchomea Mkaa




Matukio ya mauaji ndani ya familia yanayohusishwa na wivu wa mapenzi na migogoro ya mali yameonekana kushika kasi nchini. Hiyo inafuatia mwanamke mmoja Limi Shija (55) mkazi wa Kijiji cha Kabage wilayani Tanganyika, kutuhumiwa kuhusika na mauaji ya mumewe Masunga Kashinje (68) kisha mwili wake kuuzika katika shimo la kuchomea mkaa pembezoni na makazi yao.


Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Novemba 6, 2021, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Kulwa Mhoja alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akidai kuwa Kashinje alipotea katika mazingira ya kutatanisha tangu mwezi Mei 2021.



Amesema taarifa za mauaji ya Kashinje alizipata Julai 11,2021 saa 1:00 asubuhi kupitia kwa Afisa mtendaji wa kijiji hicho baada ya kumpigia simu na kumtaka afike nyumbani kwake.



“Nilipofika aliniambia kuwa jana yake alikuwa kwenye sherehe ya kanisa na huko kuna watu walimweleza kuwa kuna mtu ameuawa eneo la shimo la kuchomea mkaa. Niliwajulisha viongozi wengine wakiwamo askari wetu wa ulinzi wa jadi, sungusungu,” amesema Mhoja.



Amesema walikwenda kufanya ukaguzi kwenye shimo hilo la kuchomea mkaa wakati familia ikiwa haipo na kukuta mabaki ya binadamu jambo ambalo liliwashtua na kwenda kujadiliana.



“Mjumbe wa sungusungu, Pasi Kazimili akasema hiyo familia wameniuzia mashamba na mbuga na nimetanguliza Sh3 milioni na zingine wanadai. Nikamuuliza mliuziana kwa maandishi?, akadai hapana nashangaa wametoroka.



“Nikahoji wamehama bila kibali, Mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Kabage Mashariki, Pagi Makashi akajibu kibali nimewapa Oktoba 8,2021 wamehamia Songea. Nikamweleza mjumbe kabla ya hatua kuchukuliwa kuhusu hili tukio wafuatilie warudi ili uokoe mali zako,” amesema.



Hata hivyo, amesema wazo lake liliafikiwa na viongozi wengine na kwamba siku hiyo hiyo mjumbe aliondoka kwenda kuitafuta familia hiyo na taarifa za tukio hilo zilifikishwa ngazi zote za uongozi.



“Baada ya siku mbili kupita Polisi wa Kata walifika hapa na viongozi wa kijiji tulikuwepo tukachimba hilo shimo tukaona mwili wa binadamu ukiwa umeoza akapeleka taarifa,” ameongeza.



Amesema kwa kuwa taarifa hizo zilifika pia kwa mamlaka husika waliomba mawasiliano ya simu ya familia hiyo kisha kuanza kuwatafuta kwa njia ya mtandao.



“Oktoba 31,2021 iligundulika familia ipo Mpimbwe na makamanda wa sungusungu walifuatilia na kufanikiwa kuipata na kuileta Novemba 2, 2021 saa 11:00 jioni akiwa na watoto wake wawili,” amesema Mhonja.



Familia hiyo baada ya kufikishwa kijijini hapo ilikuta umati mkubwa wa wananchi wakiisuburi ili kupata ukweli wa suala hilo, ambapo mtuhumiwa (mke) alihojiwa na kudai kuwa hakuwa na lengo la kuua isipokuwa marehemu aliwatafuta wauaji ili wamuue yeye.



Amesema marehemu alitafuta wauaji baada ya kuwalipa Sh2 milioni ili wamuue mkewe kutokana na ugomvi wa mashamba uliokuwepo kwa muda mrefu, ambapo wauaji walipofika walibaini mkewe huyo hana hana makosa. Hata hivyo, kabla ya kufanya uamuzi mwingine mtuhumiwa huyo aliwaahidi wauaji kuwa atawaongezea Sh2 milioni ili wamuue mumewe, ambaye ndiye aliwatuma kwake.



“Wauaji walikubali fedha hizo wakamuua mumewe na kumfukia kwenye shimo hilo, baada ya mauaji Mwenyekiti wa kitongoji alimfuata mtuhumiwa na kumuomba Sh3 milioni ili awapelekee ndugu wa marehemu na kulifanya jambo hilo kuwa siri.



“Alikubali akampa pesa hiyo kufichiwa siri, aligeuka kitega uchumi ambapo viongozi wengine akiwemo wa sungusungu (jina linahifadhiwa) na mjumbe wake nao walimfuata na kumuomba Sh2 milioni ili wamtoroshe,” ameendelea kusimulia Mhonja.



Amesema viongozi hao baada ya kufika kwa mtuhumiwa walimwambia taarifa za tukio hilo wanazo hivyo, wametumwa na Kamanda wa Sungusungu awapatie fedha hizo ili wamsaidie kumtorosha asikamatwe.



“Walimwambia kuwa kama ana hizo fedha awape ili wamponyeshe kwenye hili suala, mtuhumiwa aliomba kupunguziwa malipo wakakubaliana Sh1.4 akawapa, wakamtafutia usafiri akatoroka,” ameongeza.



Mhoja amedai kuwa baada ya maelezo hayo alitoa taarifa polisi ambao walifika kwa wakati walimchukua mtuhumiwa ambaye aliwaonyesha ulipofukiwa mwili wa marehemu kisha kuondokana naye na watoto wake wawili.



Hata hivyo, tukio hilo limesababisha nyumba sita za makazi ya mwenyekiti wa kitongoji, katibu wa sungusungu na mjumbe wa sungusungu kubomolewa na wananchi wenye hasira kali kutokana na maelezo ya mtuhumiwa.



Hatua hiyo imetokana na viongozi hao kutajwa kwenye sakata hilo na mtuhumiwa kuwa walikuwa wakienda kwake kuchukua fedha ili kuficha siri.



Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Joyce Mhangwa amesema familia hiyo ilikuwa na mgogoro wa mashamba ambapo mume alitaka kuuza ili akaoe mwanamke mwingine, lakini mke na watoto wake walikataa mpango huo.



“Walichukua hatua ya kumuua, majirani walikuwa wanauliza mbona Masunga haonekani wenyewe wakawa wanadai kuwa amesafiri na baadaye nao walitoweka,” amesema Joyce.



Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu akiwa kwenye ziara yake ya kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya msingi Kabage, alikutana na kundi la wananchi wenye hasira kali wakibomoa nyumba hizo kuonyesha hasira zao hadharani.



“Nafahamu mmepata hasira kutokana na tukio hili nawaomba muwe watulivu, suala hili limefika kwenye vyombo vya sheria hivyo, mkiendelea kufanya hivi mtaishi maisha kama digi digi au sungura hatutawavumilia,” amesema Buswelu.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamini Kuzaga alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, alisema yupo safarini mkoani Arusha.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad