NGOMA nzito! Wasanii wawili wakubwa nchini Tanzania, Nasibu Abdul almaarufu Diamond Platnumz na Rajabu Abdul au Harmonize wapo kikaangoni baada ya kupeana skendo nzito ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Hivi karibuni, Diamond au Mondi alirusha kijembe kwa msanii ambaye hakumtaja akimtaka kuacha mihadarati (bangi) ambayo ni miongoni mwa makundi ya dawa za kulevya.
Katika kujibu kijembe hicho, Harmonize au Harmo, naye akaanika jambo zito kwamba msanii huyo ameona shilingi milioni 600 alizolipa ili kuondoka kwa jamaa huyo zimeishia kwenye matumizi ya unga na ndiyo maana amedhoofika mwili.
Gazeti la IJUMAA limewatafuta maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ili kujua kama wamesikia tuhuma hizo nzito na kama kuwa hatua yoyote wamechukua.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye ofisi hiyo nyeti, tayari wasanii hao wanafuatiliwa kwa ukaribu na kikosi-kazi cha mamlaka hiyo iliyo chini ya Kamishna Jenerali Gerald Musabila Kusaya.
Habari za kiintelijensia zinadai kwamba, Diamond na Harmonize ni wasanii wenye wafuasi wengi na wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa hivyo ni lazima kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo ili kupata ukweli kisha hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa kitengo hicho ambaye hakupenda kuchorwa jina gazetini, alisema jambo hilo lipo kwenye uchunguzi hivyo asingeweza kutoa habari zozote kwa kuwa siyo msemaji wa mamlaka hiyo.
Ofisa huyo anasema si mara ya kwanza kutolewa tuhuma kama hizo kwa wasanii, lakini mara zote wamekuwa wakifuatilia na kubaini ukweli.
Si mara ya kwanza kwa Diamond kuhusishwa na dawa za kulevya ambapo awali alidaiwa kuhusika na biashara hiyo haramu, lakini sasa anatuhumiwa kutumia.
Katika majibu yake, mmoja wa mameneja wa Diamond, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ aliwahi kuliambia Gazeti la IJUMAA kwamba tuhuma hizo hazikuwa na ukweli wowote ndiyo maana baada ya uchunguzi msanii huyo hakufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu mashitaka hayo.
Kwa upande wake Harmonize, mara kadhaa amekuwa akidaiwa kujihusisha na uvutaji wa bangi kiasi cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuagiza akaripoti Polisi kwa maelezo zaidi.