IKIWA ni siku moja baada ya msanii Vitali Maembe kukamatwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Bagamoyo, Chama Cha ACT-Wazalendo kimedai kuwa msanii huyo alikamatwa kwa tuhuma za kuwakashifu viongozi kupitia wimbo wake wa Kaizari.
Hayo yamelezwa leo Jumatano Novemba 3, 2021 katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalumu Taifa Chama cha ACT- Wazalendo, Mbarala Maharagande.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Maembe ambaye pia ni mwanachama wa chama hicho alikamatwa jana Bagamoyo na baadaye kuhamishiwa Kibaaha.
“Maembe ambaye jana tarehe 02, Novemba 2021 alishikiliwa na Jeshi la Polisi Bagamoyo kisha baadaye kuhamishiwa Kibaha, amehojiwa na Jeshi hilo kwa tuhuma ya kuwakashifu viongozi kupitia nyimbo yake ya Kaizari” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwanasheria wa chama hicho, Bonifasia Mapunda amefika Kibaha na kuzungumza na Maembe pamoja na uongozi Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa lengo la kufuatilia na kuhakikisha kuwa msanii huyo anaachiwa huru.
Wakati ACT-Wazalendo wakitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa waPwani, Wanko Nyigesa amesema bado wanafuatilia taarifa za kukamatwa kwa msanii huyo.
Wakati huo huo, Zitto Kabwe ambae ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, amelitaka Jeshi la Polisi kumuachia msanii huyo.
“Nawataka Jeshi la Polisi Tanzania kumwachia huru mara moja ndugu Vitalis Maembe. Polisi Mkoa wa Pwani wamefanya la hovyo sana kumkamata Vitalis kutokana na kazi ya ya kisanii ya wimbo wa Kaisari. Haivumiliki na tunataka Vitalis aachiwe huru sasa hivi,” ameandika Zitto.
Ikumbukwe kwamba Vitalis Maembe hutumia mziki wake, kueleza madhila wanayoyapata watu wa kawaida, huku akijichukua yeye kuwa sauti yao na kuwasilisha hoja hizo. Ingawa kazi yake, imekuwa ikinasibishwa na uanaharakati.
Vile vile Vitalis Maembe ni miongoni mwa wasanii waliohitimu katika wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo na kufanikiwa kupenyeza kazi zake za sanaa ndani na nje ya Tanzania. Mwaka 2020 mkali huyo wa kibao cha ‘Sumu ya Teja’ aligombea ubunge katika Jimbo la Bagamoyo kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.