Fredy Kapala shahidi wa tano wa upande wa Jamhuri katika kesi ya tuhumza za ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ametoa ushahidi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Kapala aliyejitambulisha kuwa ni mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ametoa ushahidi huo leo Jumanne Novemba2, 2021.
Ifuatayo ni sehemu ya ushahidi:
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando, Mheshimiwa Jaji kwa leo tuna shahidi mmoja lakini kabla ya kuendelea naye tuna ombi na linamuhusu shahidi mwenyewe.
Wakati wa kufile information tulimtaja kwa majina kama Frank Kapalo, na kule kwenye hatua ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi, alitajwa kama Frank Kapaa.
Usahihi ni kwamba shahidi huyu anaitwa Fredy Kapala. Hivyo tunaomba kumbukumbu za mahakama zisome Frank Kapala. Tunaleta maombi haya chini ya kifungu cha 264 (CPA) na kwa sababu ushahidi wake ulisomwa Mahakama ya Kisutu sasa tunaomba tuendelee naye.
Wakili Mtobesya utetezi: Tumesikia maombi yao na kwa kuwa ushahidi wake ulisomwa Kisutu na ndio una jina halisi hatuna pingamizi maana hiyo kasoro haimuathiri mteja wetu, hivyo hatuna pingamizi. Na mawakili wengine wote wa utetezi wanasema kuwa hawana pingamizi
Marekebisho ya jina ni kutoka Frank kuwa Fredy yaani Fredy Kapala
Huyo ndio shahidi wa tano, leo.
Jaji Tiganga: Maombi haya ya kurekebisha jina la shahidi kutoka Frank Kapala na kuwa Fredy Kapala sasa yanakubaliwa na kumbukumbu zote zitasomeka Fredy Kapala.
Shahidi anaingia mahakamani sasa na amepanda kizimbani.
Jaji anamhoji shahidi utambulisho wake.
Shahidi anaapa Sasa
Wakili Kidando: Shahidi ataongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Nassoro Katuga
Shahidi: Mimi nimeajiriwa na kampuni ya Tigo, yaani MiC Tanzania Ltd. Tigo inafanya biashara ya mawasiliano ya simu pamoja na miamala ya kifedha. Nimeajiriwa Machi 2012.
Shahidi: Nimeajiriwa kama mwanasheria wa Tigo kitengo cha Sheria. Huduma za mawasiliano inatoa kwa wateja ambao wanamiliki laini za mtandao wa Tigo
Shahidi: Wateja wa Tigo wanapatikana kwa kununua na kutumia laini za Tigo.
Shahidi: Mchakato wa manunuzi ya laini ni kwamba mtu yeyote anaweza kufika kwenye duka ama kwa wakala wa Tigo anayeziuza akiwa na kitambulisho cha Taifa au passport kwa wageni na ili laini ifanye kazi lazima ifanyiwe usajili.
Shahidi: Kwa mtu mwenye kitambulisho cha Taifa zitaingizwa namba za kitambulisho chake kwenye mashine taarifa zilizoko zitasomeka na nyingine za Nida, yaani Mfumo wa Usajili wa Utambulisho wa Taifa ambao unatunzwa na mamlaka hiyo.
Kisha ataweka alama ya kidole gumba na itasoma taarifa zote zilizoko kwenye kitambulisho na tunazichukua na kuzihifadhi kwenye mfumo wa Tigo.
Shahidi: Anayechukua taarifa hizo ni mfumo wetu ambao unawasiliana na wa Nida
Shahidi:Kuhusu miamala ya pesa, mteja akinunua laini na kuisajili anaelekeza kama anataka isajiliwe kwenye miamala ya fedha na tunampa vigezo na masharti na akikubali basi anasajiliwa kutuma na kupokea pesa.
Shahidi: Majukumu yangu mimi kama mwanasheria ni kushauri uongozi masuala yote ya sheria, kutengeneza, kusoma kupitia na kusaini mikataba, kufuatilia na kusimamia kesi zote zinazohusiana na kampuni. Kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama kupata miamala na taarifa mbalimbali za wateja.
Shahidi: Jukumu langu lingine baada ya kutoa hizo taarifa kama kuna jinsi yoyote ya kusaidia chombo chochote. Hata mtu wa kawaida anaweza kupata taarifa hizo kama akitaka.
Shahidi: Lakini mtu binafsi kupata taarifa za mtu mwingine haiwezekani
Shahidi: Mimi nina shahada ya sheria kutoka JSS Law College under Mysore University mwaka 2009. Pia nilisomea Advance Computer Course hapohapo mwaka 2007. Pia nilisomea Advance Diploma University of Dar es Salaam na pia mafunzo mbalimbali nikiwa kazini kuanzia mwaka 2012 nilipoingia kazini.
Shahidi: Nilipopata kazi moja ya majukumu yangu ilikuwa ni kutumia mifumo, hivyo ilinibidi nipate mafunzo ya wiki mpaka mwezi na nusu, nilijifunza mifumo ambayo ilikuwa lazima kuitumia.
Shahidi: Mfumo wa kwanza ulikuwa unasaidia kupata taarifa mbalimbali zilizopo, pia mfumo mwingine wa kusaidia kupata miamala.
Shahidi: Mfumo mwingine uliokuwa unaniruhusu kuangalia matumizi ya airtime ya wateja.
Shahidi: Mifumo yote ilikuwa inanisaidia katika jukumu langu la kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama kupata taarifa. Mafunzo hao yalifanyika ofisini, ofisi za Tigo zilizoko Makumbusho jengo la Derm Complex.
Shahidi: Mwaka 2015 nilipata mafunzo mengine baada ya mifumo kubadilika.
Shahidi: Katika kufundishwa mifumo tulifundishwa namna ya kupata taarifa na tahadhari za matumizi ya mifumo hiyo
Shahidi: Katika jukumu la kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama kama vile TISS, Polisi Jeshi na vinavyofanya uchunguzi.
Shahidi: Taarifa tunazozitoa ni taarifa zote zitakazokuwa zimehitajika ambazo tunazo, Kuna taarifa za kupiga na kupokea simu, taarifa ya miamala ya fedha kutuma au kupokea, bill za matumizi ya vocha, simu, usajili na nyingine zinazoambatana kama za Nida, location, ankara mbalimbali anazolipa.
Shahidi: Taarifa zote za kampuni na za wateja wake zina server yake. Kwa teknolojia ya sasa taarifa zote zinaingia moja kwa moja kwenye server hiyo.
Server ni self-generated na zinakuwa automatic saved kwenye hiyo Server.
Shahidi: Taarifa zilizoko huko ni sensitive, hivyo kuna mifumo maalumu ya kulinda hizi server na mifumo yote ambayo hizo taarifa zinapitia. Lakini pia Kuna watu ambao wanaangalia na kukagua hizo taarifa.
Shahidi: Kuna mfumo unaitwa Observed ambayo huangalia kama kuna kitu au mtu yeyote ambaye amejaribu kuingia
Shahidi: Kuna Firewalls ambao unachuna taarifa zinazoingia na kutoka.
Shahidi: Kuna Audit Trained huangalia nani kaingia wapi muda gani na kachukua nini.
Shahidi: Vulinaranilitu Access and Penetration Test. Hizi hufanywa na watu ambao ni independent profession wanaoweza kupenya na kuvunja mfumo, ili kujua kama uko safe.
Shahidi: Haya nimeyajua kutokana na mafunzo, kazi ninazofanya uzoefu wa kazi wa miaka 9 na matatizo ya kila siku.
Shahidi: Kuna vitendea kazi, kompyuta na simu ambavyo kupitia hivyo nitaombewa na kupewa access kuingia na kutumia mifumo kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu.
Shahidi: Hiyo laptop ina program ambayo inaniwezesha kuingia kwenye mifumo
Shahidi: Kuna code inayoruhusu kuingia ambayo hutolewa na mfumo wenyewe kila tu unapotaka kuingia hivyo naweza kuingia kwenye mfumo na kupata taarifa ninazozihitaji.
Shahidi: Nikishaingiza namba na kitu ninachotaka kuna button inaitwa execute inazileta taarifa nilizoziomba na kazi yangu ni kuhakiki tu kama ndicho nilichopata nazitoa kama zilivyo kwani siwezi kuzi-edit kisha nabonyeza button ya printi.
Shahidi: Kila chombo cha ulinzi na usalama au upelelezi au mahakama kinatakiwa kuwa na nyaraka ya maandishi, yaani barua yenye nembo ya mamlaka ieleze inachotaka.
Shahidi: Julai 2, 2021, nilikuwa ofisini, nilipata barua za maombi, ikitoka kwa Kamishna wa Upelelezi wa Kisayansi ikihitaji taarifa za namba ya mteja, iliyokuwa imeandikwa Julai Mosi, 2021.
Shahidi: Namba ambayo taarifa zake zilikuwa zinahitajika ni 0719933386.
Shahidi: Maombi yalikuwa mawili ambayo ni miamala ya fedha na usajili
Shahidi: Niliingia kwenye kompyuta yangu ambayo imeunganishwa na Server nikafungua Server nikaingiza namba ya simu taratibu za miamala ya fedha kuanzia Juni Mosi, 21, Julai 2020, Niliziona hizo taarifa nikaziprinti
Shahidi: Nikaingiza namba hiyo sehemu nyingine ambayo inaweza kunipa usajili
Shahidi: Siku hiyo vitendea kazi vyangu vilikuwa kwenye hali nzuri tu, na hata server iliweza kutoa hizo taarifa kwa wakati niliokuwa nahitaji.
Shahidi: Kila mtu anapata access kulingana na kazi anazofanya kama sisi idara ya sheria kutokana na majukumu yetu, pia watu wanaofanya audit wanaipata kwa kazi yao. Kuna watu wa IT security, data warehouse
Shahidi: Baada ya kuprint hizo taarifa, niliandika barua ili kujibu barua ya kamishna kile nikichokipata.
Shahidi: Kwenye zile printout nilizigonga mhuri nikaambatanisha na printout za miamala ya kifedha na usajili na barua yangu, kisha nikavipeleka ofisi ya kamishna.
Shahidi: Nikiziona hapa mahakamani hizo nyaraka naweza kuzikumbuka kwa sababu kuna barua yangu ambayo in cover letter ya Tigo, nilisaini, nikaigonga mhuri.
Shahidi: Barua niliyoletewa nitaikumbuka ni ya Julai 2, 2021, in namba niliyoifanyia kazi, na kwenye hizo printout ya miamala ya fedha niligonga mhuri na pia kuna hiyo namba.
Shahidi: Usajili nitaitambua kwa features maana nayo niliigonga mhuri wa Mic Tanzania na hiyo namba niliyopewa
Wakili Nassoro anaomba ridhaa ya mahakama amuoneshe shahidi nyaraka alizonazo na mahakama inaridhia
Wakili anamkabidhi shahidi nyaraka hizo na kumtaka aangalie ukurasa mmoja mmoja na shahidi anafanya hivyo.
Shahidi anaendelea kujibu maswali ya wakili ya kumuongoza kuhusu utambuzi wa nyaraka hizo.
Shahidi: Nimeitambua barua ya juu, ina nembo na namba na saini yangu.
Barua ya pili iliyotoka kwa Kamisha wa Upelelezi ina namba ya simu iliyoombwa.
Shahidi: Kwenye printout za miamala kuna muhuri niliougonga, kuna namba iliyoombwa na muhuri.
Kwenye usajili kuna namba iliyoombwa na mhuri.
Shahidi: Naomba mahakama hii ipokee barua niliyoipokea toka kwa Kamishna wa Uchunguzi wa Kisayansi, barua niliyomuandikia Kamishna, miamala ya fedha ya namba iliyoombewa na taarifa za usajili wa namba hiyo ziwe kielelezo cha ushahidi wangu.
Mawakili wa utetezi wanakagua nyaraka hizo kabla ya kukubali au kupinga zisipokewe mahakamani.
Mawakili wa washtakiwa wote wanasema kuwa hawana pingamizi
Mahakama imezipokea nyaraka hizo kama vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka na inaisajili kama barua ya kwenda kwa Kamishna wa Uchunguzi kielelezo namba 6.
Barua ya kutoka kwa Kamishna kielelezo namba 7, Printout ya miamala ya fedha ya namba tajwa kama kielelezo namba 8 na printout ya taarifa za usajili wa namba hiyo kama kielezo namba 9
Sasa shahidi anasoma barua yake ya majibu ya maombi ya Kamishna wa Uchunguzi wa Kisayansi kuhu miamala ya kifedha na usajili wa namba hiyo
Shahidi: Barua ya Kamishna wa Uchunguzi wa Kisayansi kwenda Tigo kuomba taarifa hizo imeandaliwa chini ya kifungu cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao.
Wakati shahidi anaendelea kusoma taarifa ya miamala ya fedha Jaji Tiganga anahoji kama miamala yote inahusika na kesi hiyo.
Jaji anashauri kama kuna taarifa ambazo hazihusiki na kesi zibaki kuwa faragha ya mteja bali Mwendesha mashtaka ajielekeze kwenye maeneo ambayo yanahusika na kesi hiyo.
Jaji anawauliza mawakili wa utetezi nao wanakubaliana na mapendekezo yake. Hivyo Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Nassoro Katuga anamuongoza shahidi kusoma miamala inayohusika na kesi hii tu.
Baada ya kusoma miamala hiyo sasa wakili anamuongoza kutoa ufafanuzi wa taarifa hizo naye anaeleza:
Shahidi: Muamala wa Julai 20, 2020 namba ya tigo 0719933386 ilituma hela kwenda namba ya Airtel kiasi cha Sh500,000 na inaonesha mnara au mahali aliyetuma pesa.
Shahidi: Ulisoma mnara wa Kinondoni na alikuwa katika kata ya Mikocheni.
Shahidi: Kuhusu usajili wa namba hiyo iliyotuma pesa imesajiliwa na inamilikiwa na Freeman Aikael Mbowe, aliyezaliwa Septemba 12, 1961.
Shahidi: Namba hiyo ilisajiliwa Februari 6, 2016. Kuna wakati aina ya usajili wa namba ulibadilika 2019 ambapo ilikuwa lazima kila mtu asajili namba yake kwa alama za vidole, ambapo aliisajili tena kwa alama za vidole Septemba 16, 2019.
Wakati shahidi anatoa ufafanuzi, wakili Katuga anarudia majibu ya shahidi jambo ambalo linamwinua wakili Mallya kupinga akidai kuwa anachokifanya wakili ni Kama yeye ndio anatoa usahidi na kwamba kama anataka apande kizimbani ili naye wamuulize maswali.
Jaji Tiganga anakubaliana na hoja ya wakili Mallya akisema kitendo cha wakili kurudia na kufafanua majibu ya shahidi kama vile mahakama haijasikia inaonekana kama wakili ndiye anatoa ushahidi na wakili Katuga anakubali na kuahidi kuacha kurudia majibu ya shahidi
Wakili Katuga amemaliza kumuongoza shahidi na kuieleza kuwa anamuacha shahidi mikononi mwa mahakama kwa ufafanuzi kama kuna maswali.
Sasa mawakili wa Utetezi wanaanza kumhoji anaanza Wakili Jeremiah Mtobesya.
Mtobesya: Nimekusikia ukisema Kuna wakati mifumo yenu inaweza kuingiliwa na hackers, ni sahihi?
Shahidi: Ni sahihi
Wakili wa utetezi: Hackers ni watu gani mwambie Jaji
Shahidi: Ni watu wa kawaida wanaosoma mfumo na kuhufahamu na kujaribu kuingia kwenye mfumo kuchukua au kuharibu taarifa au mfumo.
Mtobesya: Sasa nitakuwa sahihi wakati anakuongoza wakili Katuga mpaka una-generate hizo taarifa kulikuwa na possibility ya hackers kuingilia taarifa hizo?
Shahidi: Sikusema
Mtobesya: Nitakuwa sahihi nikisema hacker’s wanauwezo wa kuingia na kucheza na mfumo
Shahidi: Uwezekano upo
Mtobesya: Ofisini kwenu kuna wanasheria wangapi?
Shahidi: Watatu.
Mtobesya: Ofisi ya Tigo umesema ni ofisi au
Shahidi: Jina la biashara
Mtobesya: Ofisi ya Tigo ina wanasheria wangapi:
Shahidi. Watatu
Mtobesya: Ni sahihi nikisema hii taarifa hukuifanyia kazi wewe, ni kielelezo gani kitakachokutambusha?
Shahidi: Kuna barua
Mtobesya: Lakini haina jina lako
Sahahidi: Ndio
Mtobesya: Nitakuwa sahihi kwa mujibu wa kielelezo cha 9, taarifa za usajili aliyesajili laini ya huyu uliyemuita Aikael Freeman Mbowe hazipo?
Shahidi: Zipo
Mtobesya: Taarifa zinasajiliwa na Nani?
Shahidi: Device
Mtobesya: Kuna jina la mwenye device hapa?
Shahidi: Halipo
Sasa ni Wakili Mallya anamhoji shahidi
Wakili Mallya: Tigo umeajiriwa lini?
Shahidi: 2014
Wakili Mallya: Umeajiriwa kwenye department gani?
Shahidi: Legal department
Wakili Mallya: Taarifa za Tigopesa na usajili zinashughulikiwa na department
Shahidi: Ulinzi
Wakili Mallya: Shahidi wewe unakaa na wenzako vizuri?
Shahidi: Nawafahamu
Mallya: Kwenye hiyo department ya IT Security Kuna Yahya Zahoro ndio anashughulika na Investigation?
Shahidi: Yahaya Zahoro ni internal auditor.
Wakili Mallya: Ulizungumza kitu kinaitwa tell pin
Shahidi: Ndio
Wakili: Ni nini?
Shahidi: Ni mfumo unaohusiana na masuala ya Tigopesa
Wakili Mallya: Wakati unatoka ushahidi kuhusu kielelezo namba 8 uliieleza mahakama umeprinti kutoka kwenye mfumo gani.
Shahidi: Ndio
Wakili: Ni mfumo gani unatumia
Shahidi: Inategemea
Wakili Mallya: Wakati unaona hizi taarifa kwenye kompyuta yako ulitumia mechanism gani kuifanya iwe printed?
Shahidi: Niliprint
Wakili Mallya: Ulisema ujuzi umepata kutokana na uzoefu, mafunzo na changamoto za kazi ulimweleza Jaji ni changamoto gani ulikuwa unapata?
Shahidi: Hapana
Wakili Mallya: Huyu mtu unasema anaitwa Freeman Mbowe kwenye maelezo taarifa umetaja kilimanjaro umeielezea mahakama?
Shahidi: Hapana
Wakili Mallya: Kilimanjaro kuna jiji
Shahidi: Hapana
Wakili Mallya: Huyu Mbowe alisajili mwenyewe?
Shahidi: Wakili anashindwa kuelewa hizi taarifa tulizuchukua Nida
Wakili: Hii nyaraka imetoka kwenu au Nida
Shahidi: Nida
Wakili: Aliyemsajili Mbowe nani?
Shahidi: Simjui
Wakili Mallya: Kwa kuwa taarifa za aliyemsajili Mbowe hazipo, kwa hiyo Mbowe alijisajili mwenyewe, nipo sahihi?
Shahidi: Hauko sahihi
Wakili Mallya: Ukiombwa taarifa za mimi na rafiki yangu tunatumiana pesa utatoa au hutoi?
Shahidi: Sitatoa
Wakili: Ulipoombwa taarifa za Mbowe ulihoji ni za nini
Shahidi:Sikuhoji
Wakili: Ukiwa kama mwanasheria hukuona sababu ya kuhoji kosa?
Shahidi: Sio sehemu ya majukumu yangu.
Wakili Mallya: Kwanini hukuuliza Mbowe ana kosa gani ukatoa taarifa
Shahidi: Kwanza wakati zinaombwa sikujua ni nani, niliona tu namba na kuifanyia kazi.
Wakili Mallya: Mheshimiwa Jaji ni hayo tu.
Jaji. Tuna break kwa dakika 40 tutarudi 8.00 mchana