Mwandishi wa Habari avunjika Mguu akijiandaa kwenda Kanisani kufunga Ndoa




Mwandishi wa Habari na mtangazaji wa redio habari njema Mbulu Manyara Agustino Hamis na mpenzi wake Magreth wamelazimika kufunga ndoa yao Hospitalini baada ya kupata ajali akielekea Salun kujiandaa na maandalizi ya ibada ya ndoa na kuvunjika mguu.

Agustino na Magreth licha ya kutokea kwa changamoto hiyo wamehakikisha wanatimiza azma hiyo ya kufunga ndoa.

'Naomba shamrashamra zote mlizokuwa nazo ziendelee, mimi nipo pamoia nanyi,naomba muwe na furaha"alisisitiza Agustino akiwa kitandani.

Kwa upande wake bibi harusi pia anasema kuwa asingeweza kuahirisha harusi.

Wakati wa ndoa yao ya katika hospitali ya Lutheran Karatu novemba 20 mwaka huu wa 2021, wanandoa hao mbele ya Padri, wazazi na baadhi ya mashuhuda, walivishana pete na kuapa kupendana daima katika hali yoyote.

Ndugu wanasema Saa chache tu kabla ya kwenda Kwenye shughuli hiyo muhimu, Agustino akiwa katika usafiri wa pikipiki kuelekea salun akiendeshwa na nduguye, walipata ajali eneo la Rhotia chini mita chache kabla ya kufika barabara kuu ya kuelekea Karatu mjini ambapo walikuwa wakijaribu kulikwepa gari lililokuwa mbele yao na matokeo yake kuanguka na mguu wake ukavunjika na kupata majeraha Kwenye mkono.

"Agustino anasema tukio hilo litabaki kuwa historia katika maisha yake na mkewe na kwamba anamshukuru Mungu kwani yupo Salama.

Mshehereshaji ambaye alitoka Babati kwa ajili ya shughuli hiyo Lucas Mondu (Mc Luca) anasema kuwa wakati anatoka Babati asubuhi waliwasiliana na Bwana harusi na alipofika Rhotia alijaribu kumpigia ili amweleze kuwa ameshafika lakini alijibiwa na mtoa huduma wa mtandao kwamba mteja hapatikani kwa sasa, anasema alijaribu kufanya hivyo mara nyingi bila mafanikio.

Anasema baadaye wakati anawaza afanye nini akasikia wapita njia wanasimuliana juu ya ajali iliyomhusisha Bwana harusi na alipouliza aliambiwa mhusika ni Agustino Hamisi.

'Nilishikwa na butwaa ila nikajikaza na kuomba kuelekezwa nyumbani ambapo bodaboda alinipeleka na baadaye tukaanza safari ya kuelekea hospitali mimi na wanafamilia.

Mc Lucas anasema ni mara yake ya kwanza anasherehesha katika mazingira ya hospitali.

Anasema shughuli aliyoifanya Hospitalini hapo kama mshehereshaji ni kuongoza zoezi la kukata keki ambayo iliongozwa na Bwana harusi na Bibi harusi na kisha wakawalisha wazazi wao na ndugu wengine huku nyuso zao zikiwa na furaha.

Baada ya zoezi la keki na Picha mbalimbali za kumbukumbu sherehe ilihamia nyumbani kwao Rhotia ya juu ambapo meza kuu alikuwa Bibi harusi na wasimamizi.

Sherehe iliendelea kama kawaida kwa ndugu,marafiki na majirani kufurahi kwa pamoja kwa kula na kunywa.

Hata Hivyo Agustino anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mkuaranga iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha na hali yake inaendelea kuimarika kwa mujibu wa taarifa za karibu tulizozipata leo Novemba 21.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad