Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba amesema Sh1.3 trilioni za IMF, ndiyo mkopo wa kwanza kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo amesema Watanzania wakae mkao wa kula kwa kuwa kazi inayokwenda kufanyika ni ya kihistoria.
Dk Mwigulu ameliambia Bunge leo wakati akihitimisha mjadala wa Serikali katika hoja yake ya mapendekezo ya mwongozo wa mpango wa Maendeleo wa Serikali kwa mwaka 2022/23.
Amekanusha taarifa za kuwa tangu Rais Samia alipoingia madarakani kwamba ameshakopa zaidi ya Sh94 trilioni akasema huo ni uongo na uzushi.
"Kwa Serikali ya awamu ya sita, Sh1.3 trilioni kwa mama ndiyo mkopo wake wa kwanza na hivi sasa tuko katika mazungumzo mazuri huenda yakawa na masharti nafuu kabisa," amesema Mwigulu.
Kuhusu madeni amesema Serikali haijawahi kukopa kwa ajili ya kulipa mishahara au kujaza mafuta bali wanakopa kwa ajili ya kufungua miradi.
Kuhusu miradi amesema Serikali itaendelea kukopa pale inapoona panafaa kufanya hivyo hasa kwenye miradi ya kimkakati kwa lengo la kuifungua nchi.