Taifa limeendelea kudanganywa kwa mara nyingine ,naweza kusema hivyo bila shaka. Pia, udhaifu wa wachambuzi wetu katika kulipokea jambo fulani kisha kulifanyia utafiti wa kina kabla ya kulizungumza ,limewekwa kapuni. Inahuzunisha kwa upande mmoja.
Kama Taifa inapofikia hatua hii, hatuna budi kujitazama upya. Taifa hili si Taifa la wendawazimu...Taifa hili sio Taifa la Vilaza.
Katika maendeleo ya utandawazi wa teknolojia yanayoibadilisha Dunia kila kukicha, ni kazi rahisi kudanganya na ni kazi ngumu vile vile kuficha ukweli...Kwanini?
Wiki hii klabu ya Simba ilimtangaza raia wa hispania aitwaye Pablo Franco Martin kuwa kocha wao mpya akichukua nafasi ya Didier Da Rosa aliyekatishiwa mkataba wake.
Hapana shaka kuwa, Pablo Franco Martin ni kocha msomi mwenye lesen ya Uefa A Pro. Leseni yake ni ya kiwango cha juu Barani Ulaya. Leseni hii katika madaraja ipo sawa na ile ya CAF A kwa upande wa Bara la Afrika.
Makocha wenye ngazi ya leseni hii ,utazamwa kuwa wakufunzi wa wanafunzi wa fani ya ukocha kwa wakati mwingine. Bila shaka yoyote,Pablo Franco Martin amejaza vyeti katika fani hii.
Pamoja na wasifu wa elimu yake, nimejikuta nikibakia na mshangao baada ya kusikia wasifu wa Pablo Franco Martin kuwa amewahi kuwa msaidizi wa Julen Lopetaqui kunako klabu ya Real Madrid. Kwanini nishangae?
Kwanza napenda utambue mgongano wa kimaslahi katika makala hii. Mtoa makala ni shabiki kindaki ndaki wa Real Madrid kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Kuwa shabiki sio kigezo cha kujua mengi kuhusu Real Madrid, ila mimi naweza kusema ni zaidi ya shabiki kwa uwanja wa kuifuatilia kila habari ya timu hii...Je kuna tatizo kwa Pablo Franco Martin?
KAMA TAIFA LIMEDANGANYWA...
Niliposikia jina la Pablo Franco Martin katika wasifu wa kuwahi kuhudumu kama kocha msaidizi wa Real Madrid kati ya Julai 31, 2018 hadi November 2, 2018, nilijiuliza maswali mengi...
Moja ..Hili ni jina geni katika masikio yangu kuwahi kulisikia ndani ya viunga vya Charmatin zilipo ofisi za Real Madrid jijini Madrid na katika viwanja vya Valdebebas mahala ambapo timu ya Real Madrid wanapofanyia mazoezi.
Pia ,jina hili ni geni kunako kiwanja cha Alfredo Di Stefano mahala ambapo Real Madrid Castilla (Madrid B) wanapoutumia kwa mechi zao.
Pia ,jina la Pablo Franco sio jina lenye maana kubwa ndani ya majukwaa la dimba la Santiago Bernabeu. Hii ina maana gani?;
PABLO FRANCO MARTIN HAJAWAHI KUWA KOCHA MSAIDIZI WA REAL MADRID
Huu ndio ukweli uliofichwa ama unaofichwa makusudi na baadhi ya watu kwa maslahi yao.Mtu huyu anayetajwa kuwa amewahi kuwa kocha msaidizi kunako klabu ya Real Madrid ...ukweli hajawahi kuwa kocha wa Real Madrid ama kuwa mfanyakazi wa kawaida wa klabu ya Real Madrid.
Bahati mbaya porojo hizi, zimewaingia wachambuzi wetu vijana na wakongwe na kuonesha udhaifu mkubwa wa kulipokea jambo na kutolifanyia utafiti kwa kina. Uamuzi kama huu unaweza gharimu Taifa kwa wakati mwingine.
Uthibitisho wao (wachambuzi)ukapokelewa na mashabiki wa soka nchini na kila mmoja akizungumza wasifu huo bila kujua kuwa sio kweli.
Bahati mbaya hata wachambuzi wetu wakubwa nao wakajikuta wakiingia katika mkumbo huo. Wakatangaza kuwa Pablo Franco Martin alipata kuwa msaidizi wa Julen Lopetaqui kunako klabu ya Real Madrid....
UKWELI NI UPI SASA ?
Mnamo Julai 1, 2018..Real Madrid walimtangaza Julein Lopetaqui kuwa kocha wa klabu hiyo. Lopetaqui alichukuliwa toka timu ya Taifa ya Hispania na uamuzi wake huo ukapelekea mkataba wake na Chama cha soka cha Hispania ufikie tamati wa kuifundisha timu ya Taifa. Lopetaqui akaenda zake Real Madrid kwa madaha!
Real Madrid alienda naye Albert Celadez (Huyu ni mchezaji wa zamani wa Real Madrid) ambaye ndiye alikuwa kocha msaidizi namba moja kwa Julen Lopetaqui kunako klabu ya Real Madrid.
Huku msaidizi mwingine wa Lopetaqui alikuwa Pablo Sanz Iniesta. Huku kocha wa Makipa akiwa Juan Canales, msaidizi wake aliitwa Antolin Gonzalo. Timu ya makocha wa viungo ilikuwa chini ya Antonio Pintus (huyu alikuwa hapo tangu enzi ya utawala wa Zinedine Zidane) akiwa mkuu, huku akisaidiwa na Jose Conde, Javier Mallo (Mkufunzi wa viungo na msomaji wa wapinzani), na Oscar Caro. Hili ndio benchi la ufundi la Real Madrid chini ya Julein Lopetaqui.
Benchi hili la ufundi lilihudumu kunako Real Madrid kuanzia Julai 1, 2018 hadi October 28,2018.. na siku moja baadae yaani October 29,2018 baada ya kipigo toka kwa FC Barcelona.
Lopetaqui na benchi lake walifukuzwa kazi isipokuwa kwa Antonio Pintus na Javier Mallo pekee. Hawa wawili waliendelea kuwapo Real Madrid.
Miezi mingi baadae, Albert Celadez alikuja tangazwa kuwa kocha wa Valencia huku Julen Lopetaqui akiwa kocha wa Sevilla yupo na Pablo Sanz Iniesta, Oscar Caro hadi hivi leo.
Ikumbukwe kuwa Albert Celadez ndiye alikuwa kocha msaidizi wa Julen Lopetaqui tangu akiwa FC Porto, kisha wakakutana tena timu ya Taifa ya Hispania.
Albert Celadez akiwa kocha wa Timu ya Taifa ya Vijana na Lopetaqui akiwa kocha wa timu ya wakubwa. Lopetaqui akamfanya kuwa msaidizi wake nambari moja kwa timu ya Taifa ya wakubwa.
Baadae waliondoka wote na kuungana kunako klabu ya Real Madrid.. walipohudumu kwa siku 120 tu kabla ya kufukuzwa.
Julen Lopetaqui na msaidizi wake Albert Celadez waliishia kuiongoza Real Madrid katika mechi 14 tu. Wakishinda 6 wakitoa sare mechi 2 na kufungwa 6.
NI KWELI ALIKUWA MSAIDIZI WA SANTIAGO SOLARI KWA MECHI MOJA HAPO HAPO REAL MADRID?
Inachekesha wakati mwingine. Pablo Franco Martin sio tu hajawahi kuwa kocha msaidizi wa Real Madrid bali pia kufanya kazi kwenye sekta yoyote klabuni hapo.
Alipofukuzwa Julen Lopetaqui. Real Madrid ilimpandisha kocha wao wa timu ya vijana Santiago Solari ambaye pia alimteua Santiago Sanchez kuwa msaidizi wake mara moja.
Hivyo kuanzia October 29, 2018 kocha mkuu wa Real Madrid alikuwa Santiago Solari na msaidizi wake namba moja aliitwa Santiago Sanchez na meneja msaidizi aliitwa Jose Parrales (Msaidizi namba mbili) . Kocha wa makipa alikuwa Robert Vazquez. Huku Antonio Pintus na Javier Mallo waliendelea kuwa makocha wa viungo.
JE UDANGANYIFU HUU UMEANZIA WAPI?
Wasifu wa Pablo Franco Martin kuwa alipata kuwa kocha msaidizi wa Real Madrid, upo kwenye midomo ya wachambuzi wa soka wa Kitanzania na baadhi ya ripota wa habari za soka wachache wa wa kiafrika waliopokea habari kama ilivyo toka nchini kwetu.
Huku pia wasifu huu ukiwa umechomekwa katika mitandao ya "wikipedia na transfer Market " pekee. Mitandao hii miwili mtu yoyote yule ukiwa na account unaweza kurekebisha kwa kupunguza ama kuongeza taarifa bila vikwazo.
Mfumo huu unaifanya wavuti hizi isiwe cha nzo cha uhakika cha kuamini wala kuchukuliwa kama rejeo (reference) na haitambuliki kwenye mifumo ya ushahidi wenye kuthibitisha Duniani kote.
Jina la Pablo Franco Martin halipo kwenye list ya watu waliowahi kuwa makocha wasaidizi wa klabu ya Real Madrid zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Inashangaza kuwa jina la Pablo Franco Martin halipo kwenye wavuti, kurasa rasmi za klabu ya Real Madrid za mitandaoni.
Kitu kingine kinachoshangaza pia...Huyu Pablo Franco hata uliandike jina lake "Google" hatambuliki kama aliwahi kuwa kocha wa Real Madrid tofauti na wavuti hizo nilizozitaja.
Katika picha za pamoja za benchi la Ufundi lililotangazwa mwezi Agosti ,2018 na Real Madrid chini ya Julen Lopetaqui halipo jina Pablo Franco Martin wala picha yake...hata katika benchi la ufundi la Santiago Solari halipo jina lake wala picha yake. Unajiuliza inakuwaje?
Wanajua kucheza na fursa..wanajua kucheza na hisia zenu. Mwisho wanajua nini tunataka..
Nyuma ya Pablo Franco Martini katika ujio wake kuja Simba, wako watu wanaojua nini wanafanya...ni wenye akili mno. Niwapongeze katika hilo.
Walianza kucheza na wavuti zile ambazo wabongo wengi tunakimbilia kama wikipedia, kisha transfer Market....walipofanikiwa hapa...wakajua kabisa hata wachambuzi wetu wataishia hapa.
Wachambuzi wetu hawakutaka kuzisumbua akili zao. Hata kujaribu kufuatilia je ni kweli aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Lopetaqui kunako Real Madrid?
Hawakujaribu hata kutafuta picha zake akiwa kwenye benchi la Real Madrid na wachezaji.
Kama hakuna...katika kila klabu na kila kocha mpya anapokuja kuna utaratibu wa picha rasmi la benchi la ufundi je Pablo Franco Martin yupo?..Hakuna.
Porojo zile zile za Inonga Baka kuitwa timu ya Taifa ya DRC wakati sio kweli ndio hizi hizi za Pablo Franco kuwahi kuwa msaidizi wa Real Madrid. Wakati si kweli...Inahuzunisha!
Hata Pablo Franco Martini mwenyewe hajui kama aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Julen Lopetaqui kunako Real Madrid..ujue
Ukitaka uthibitisho wa wasaidizi hawa tafuta kurasa rasmi za Real Madrid, wavuti yao, na google kwa ushahidi wa picha hata kutazama youtube ila kote huko hayupo Pablo Franco Martin...Hizi habari za Pablo franco kwa Real Madrid ni Propaganda tu.
NB:Makala haya yameandikwa na shabiki wa mpira,na klabu ya Real Madrid.
Original Article: Soka la Bongo