Ngoma ngumu kesi ya Mbowe na wenzake





Mawakili wanaomtetea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na makosa ya ugaidi jana walipata ahueni kwa mara ya kwanza pale mahakama ilipokataa kupokea kitabu cha kumbukumbu za mahabusu kama kielelezo cha kesi hiyo.


Jaji Joachim Tiganga alikataa kupokea kilelezo hicho baada ya kuridhika na hoja za utetezi kuwa shahidi aliyetaka kukitoa alishindwa kueleza ni kwa namna gani kilimfikia.



Uamuzi huo umekuja kufuatia pingamizi la utetezi lililowekwa juzi wakati wa usikilizwaji wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.



Kesi hiyo inamkabili Mbowe na watu wengine watatu waliowahi kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi cha makomandoo, Ngerengere, kabla ya kuachishwa kazi kwa sababu za kiafya.



Kesi hiyo ndogo iliibuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga kupokewa kwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohamed Ling’wenya kwa madai kuwa hakuwahi kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam anakodaiwa kuchukuliwa maelezo.



Mawakili hao walidai pia mshtakiwa huyo alilazimishwa kusaini maelezo yaliyokuwa yameandaliwa huku akitishwa.



Hali hiyo iliibua mabishano ya kisheria juzi kati ya mawakili wa Jamhuri na wale wa utetezi kiasi cha Jaji Tiganga kuahirisha kesi hiyo hadi jana kwa kutoa uamuzi wa pingamizi hilo.



Upande wa mashtaka ulimleta Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, Jumanne Malangahe kuipa nguvu kesi yao kuwa Ling’wenya alihojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa kuwa ndiye aliyedai kumtoa mahabusu ya kituo hicho kwa ajili ya mahojiano.



Alieleza katika ushahidi wake kuwa ndiye aliyejaza kitabu cha kumbukumbu za mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.



Akisoma uamuzi huo, Jaji Tiganga alisema: “Ni kweli kwamba (shahidi) hajaeleza ametoa wapi (kielelezo). Na kuhusiana na chain of custody (mnyroro wa utunzaji kielelezo), shahidi hajaeleza chain of custody; kwamba ni kwa namna gani kielelezo hicho kimemfikia.



“Ni kweli kwamba kielelezo kipo kwenye kumbukumbu ya shauri lingine. Ili mahakama ione kama kilifuata utaratibu, kilipaswa kionekane kilifuata utaratibu wa kiutawala kutoka mahakamani.



“Na kwa namna hiyo, kielelezo kinajifuta chenyewe kwa sababu shahidi hakuonyesha namna gani kilimfikia. Assumption (inachukuliwa) ni kwamba kielelezo kipo kwenye chumba cha mtunza kielelezo cha mahakama. Hakuna ushahidi kwamba shahidi alikipataje kuja mahakamani



“Kwa sababu hiyo, mahakama inakikataa kielelezo hiki. Natoa amri,” alisema Jaji Tiganga.



Ikumbukwe kuwa tangu kesi hiyo ianze, mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa na wa tatu Mohammed Ling’wenya waliodaiwa kukamatwa Moshi, wamekuwa wakisisitiza hawajawahi kufikishwa kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.



Lakini upande wa mashtaka umekuwa ukidai kuwa mara tu baada ya kukamatwa Moshi, Ling’wenya na Adam Kasekwa walisafirishwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam na kuhojiwa.



Upande wa mashtaka ulimleta Jumanne ili ushahidi wake uunge mkono ushahidi huo, kwamba yeye ndiye aliyemhoji mshtakiwa wa tatu.



Ushahidi wake katika kesi ndogo ulilenga kuonyesha kuwa yeye ndiye alimtoa mahabusu kwa ajili ya mahojiano na alijaza kitabu cha kumbukumbu ya mahabusu.



Baada ya uamuzi wa jana, Jumanne aliendelea na ushahidi wake ndani ya kesi ndogo inayohusu uhalali wa maelezo ya mshtakiwa wa tatu, Ling’wenye huku akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.



Shahidi huyo aliieleza mahakama kwa kirefu jinsi alivyomchukua mshtakiwa Ling’wenya hadi kwenye chumba cha mashtaka cha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam Agosti 7, 2020 kwenda chumba cha mahojiano alipochukua maelezo yake ya onyo.



Baada ya kumaliza kuyasoma maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, shahidi aliiomba mahakama iyapokee kwa ajili ya utambuzi na kuwa kielelezo cha kwanza katika kesi hiyo ndogo.



Baada ya hatua hiyo yakafuata mahojiano na mawakili wa utetezi.



Wakili Jeremiah Mtobesya: Shahidi wakati mnamkamata mlikuwa na taarifa gani?



Shahidi: Mohammed Ling’wenya alikuwa ni miongoni mwa kikundi cha waliokuwa wanapanga kula njama kufanya vitendo vya ugaidi kulipua vituo vya mafuta, maeneo ya mikusanyiko, kudhuru viongozi na kukata miti kuzuia barabara.



Mtobesya: Mlimakamata lini Ling’wenya?



Shahidi: Agosti 4, 2020



Mtobesya: Utakubaliana nami kuwa unapokwenda kupeleleza unakuwa tayari na taarifa?



Shahidi: Ndiyo.



Mtobesya: Lini uliandika maelezo ya Ling’wenya?



Shahidi: Agosti 7, 2020.



Mtobesya: Unaelewa maelezo ya onyo yanachukuliwa kwa njia gani?



Shahidi: Wakati zinapaptikana taarifa za kuwa anahusishwa na kwenda kutenda makosa.



Mtoibesya: Nitakuwa sahihi nikisema maelezo ya onyo yanataka mtuhumiwa aelezwe ni kosa gani anatuhumiwa nalo.



Shahidi: Ni sahihi.



Mtobesya: Tusaidie kitu kimoja. Ni kwa nini hamkuchukua maelezo ya mtuhumiwa akiwa Moshi na mkaja kuchukua maelezo ya mtuhumiwa siku tatu baadaye, tena akiwa Dar es Salaam?



Shahidi: Ni kwa sababu za kipelelezi na tulikuwa tunaendelea kutafuta watuhumiwa wengine na mshtakiwa huyu naye alikuwa ni sehemu ya kutusaidia kuwapata washtakiwa wengine. Sababu nyingine ni kutokana na nature ya jalada hili lilikuwa limefunguliwa Dar es Salaam.



Mtobesya: Mweleze jaji kama kuna kanuni yoyote au takwa la kisheria ni lazima maelezo ya mshtakiwa yaandikwe sehemu lilipofunguliwa jalada au ni uzoefu wenu tu katika utendaji kazi, ambao mmeufanya kuwa kama sheria?



Shahidi: Sio kanuni.



Wakili John Mallya: Tuambie unakifahamu Kituo cha Polisi Mbweni?



Shahidi: Nakifahamu.



Mallya: Ni sahihi kituo hicho cha polisi ni cha Wilaya ya Kawe?



Shahidi: Sifahamu mpaka nijiridhishe.



Mallya: Kwa hiyo wakati unawapeleka watuhumiwa Mbweni ulikuwa hujui kama ni kituo kikubwa cha kipolisi Kawe?



Shahidi: Hicho ni kituo kama vingine.



Jaji: Sauti yako Mallya ipo juu sana, jitahidi kuidhibiti. (kicheko mahakamani).



Mallya: Sawa mheshimiwa jaji, nitajitahidi kupunguza lakini pia wasikie washtakiwa ninachohoji.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad