Pablo Awaduwaza Mastaa Simba Kuwapa Mazoezi Kidigital



YANGA, Azam, Biashara zote maji yalizidi unga. Simba ndiyo klabu pekee ya Tanzania iliyosalia kimataifa na Kocha Pablo Franco amewaduwaza mastaa wake kwa kuwafundisha kidigitali zaidi.

Wamepiga tizi la maana wiki hiii na sasa wako fiti kukiwasha Jumapili dhidi ya Red Arrows ya Zambia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni mechi ya Shirikisho kuwania kutinga hatua ya makundi.

Ili kuwamaliza mapema Wazambia hao, kocha mkuu wa chama hilo, Pablo Franco akishirikiana na wasaidizi wake Seleman Matola na Thierry Hitimana sambamba na kocha wa viungo Don Daniel De Castro kutoka Hispania wameendelea kutengeneza kikosi cha mauaji ambacho kitaleta heshima Msimbazi. Mwanaspoti limekuwa mazoezini na kambini kwa Simba kila siku likifuatilia mazoezi yanayoendelea asubuhi na jioni katika Uwanja wa Mo Simba Complex, Bunju na kukuletea ukweli ulivyo.

Kocha Pablo na wasaidizi wake huko mazoezini wamekomaa na ufundi katika maeneo yote kwa maana ya makipa, mabeki, viungo na washambuliaji huku wakihimiza kupiga pasi za uhakika na kushambulia kwa spidi.

KOCHA AWADUWAZA MASTAA

Mastaa wa Simba juzi waliduwaa baada ya Kocha Pablo kuanza kuwafundisha kwa staili adimu ambazo hawakuwahi kuzizowea siku za nyuma hata kwenye makuzi yao ya kisoka.

Ameonesha kuwa hataki masihara kwenye kazi yake baada ya kutinga mazoezini na kompyuta mpakato ‘Laptop’ aina ya Aple na kuitumia kuwaelekeza mastaa wake namna ya kucheza kwa picha na video kama njia ya kusisitiza kila anachokieleza wamuelewe zaidi kwa kuona picha na vitendo.

Licha ya kukataa tukio hilo lisipigwe picha wala kuonekana kwa ukaribu na mashabiki, juzi jioni baada ya kufika Uwanjani, aliwakusanya wachezaji wote katikati ya Uwanja na kuwasha Laptop kisha kuwapa somo nini wanatakiwa kufanya kama kwa dakika 10 hivi kisha wakaanza kwa vitendo.

Hapo nyota hao wa Simba wakiongozwa na nahodha John Bocco walienda moja kwa moja kwa kocha wa Viungo Castro na kupasha mwili joto kabla ya kwenda kufanya yale matizi waliyoelekezwa kwenye Laptop.

Baadae Pablo aligawa Uwanja mara mbili na ambapo kila nusu ya uwanja ilikuwa na timu mbili zikicheza kama mechi huku makocha Pablo, Matola na Hitimana wakihimiza kupiga pasi za kwenda mbele haraka haraka na kufunga.

Meddie Kagere, Rally Bwalya, Bernard Morrison, Pape Sakho, Ibrahim Ajibu, Yusuph Mhilu na Peter Banda na Dancun Nyoni walionekana kuiva na kuendana na mbinu hizo.

Wakati huo mabeki Henock Inonga, Paschal Wawa, Kennedy Juma, Joash Onyango, Mohamed Hussein, Gadiel Michael, Israel Mwenda na Shomari Kapombe nao walikuwa wakitimiza majukumu yao kwa umakini.

Baada kama ya dakika 20 za mazoezi hayo, Pablo aliwaita tena wachezaji wote na kuwasha Laptop na kuwaonyesha maelekezo mengine kwa njia ya picha na video na baada ya muda akawarudisha tena uwanjani kufanya hadi pale alipojiridhisha kuwa wameiva.

SAKHO, INONGA WAPANGUA KIKOSI

Kupona kwa mshambuliaji Pape Sakho na uwepo wa beki kisiki Inonga ‘Varane’ huenda kukapangua kikosi cha Simba kutokana na ubora wanaouonesha mazoezini na tayari kocha Pablo ameanza kuwaweka kwenye kikosi chake.

Kwa mujibu wa mazoezi ya juzi na jana, Sakho na Varane walikuwa panga pangua katika kila programu huku wakionesha ubora mkubwa wa kuanzisha mashambulizi, kukaba, kuziba nafasi na kuupanga ukuta kwa upande wa Inonga huku Sakho akiteka uwanja kwa chenga, spidi, pasi na mashuti mazito ambayo mengi yalizaa mabao. Wawili hao huenda wakaanza kwenye mechi ya Jumapili kwani katika kikosi kilichokuwa pamoja kwa muda mrefu katika mazoezi, Pablo aliwaanzisha Aishi Manula, Kapombe,Tshabalala, Onyango, Varane, Jonas Mkude, Bwalya, Mzamiru Yassin, Kagere, Sakho na Morrison ambao walikuwa wanaupiga mwingi. Kibu Denis anaonekana kutokuwa kwenye chaguo la kwanza.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad