Dodoma. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameeleza mafanikio ya Serikali katika miaka 60 ya Uhuru, huku akitaja namna alivyopata wakati mgumu kushughulikia vichwa 13 vya treni vilivyokutwa bandarini mwaka 2017.
Uwepo wa vichwa hivyo ambavyo vilidaiwa kutokuwa na mwenyewe, uliibuliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, kabla ya baadaye Serikali kulazimika kuunda timu ya wataalamu 11 kufanya tathmini ya ubora wake na thamani ya fedha kwa lengo la kuvinunua vichwa hivyo.
Akizungumza na wanahabari jijini hapa jana, Waziri Mbarawa alisema baada ya Serikali kuvinunua vichwa hivyo kwa ajili ya matumizi, sasa vimekuwa na msaada mkubwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Profesa Mbarawa alisema jana kuwa, tatizo la vichwa hivyo lilitokea wakati yeye akiwa waziri na hakuwa na majibu, na alipowauliza watendaji wake kuhusu mmiliki wa vichwa hivyo, pia hawakuwa na majibu.
“Ilinipa shida sana, maana TRC walisema hawana taarifa na upande mwingine hawakuwa na majibu, sasa nikabaki najiuliza nini maana yake,” alisema Profesa Mbarawa.
Hata hivyo, alisema baadaye walikuja kubaini kuwa vichwa hivyo vilikuwa ni mali ya TRC isipokuwa mkataba wa ununuzi kati ya shirika na watengenezaji ndiyo uliokuwa na tatizo kwa sababu waliwahi kuviingiza nchini kabla ya muda.
Azungumzia mafanikio
Akizungumzia sekta ya ujenzi na uchukuzi tangu 1961, waziri huyo alisema kumekuwa na mafanikio makubwa ambayo nchi imeyafikia tangu nchi ilipoanza kwa bajeti ya Sh2.1 bilioni hadi kufikisha Sh 1.5 trilioni mwaka wa fedha wa 2021/22.
Alisema kwa sasa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), unamiliki mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilometa 36,361.88 ambapo kilomita 12,215.51 ni barabara kuu na kilomita 24,146.37 ni barabara za mikoa.
“Barabara kuu za lami ni kilomita 9,058.2 na za mikoa ni kilomita 2,218.22, lakini mtandao wa barabara nchini umekuwa ukiboreshwa na kuongezewa kwa kuweka mkazo katika ujenzi wa barabara kuu, mikoa, wilaya na madaraja,” alisema Profesa Mbarawa.
Pamoja na kuunganisha makao makuu ya mikoa, Serikali imefanikiwa kujenga mtandao wa barabara zinazounganisha nchi jirani za Msumbiji, Kenya, Uganda, Rwanda na Zambia.
Alisema mwaka 1961 wakati nchi inapata Uhuru, wahandisi wazawa walikuwa wawili, lakini hivi sasa wamefikia 32,145 , huku Serikali ikiendelea kuwajengea uwezo wahandisi hao kupitia Bodi ya Makandarasi (CRB).
Viwanja vya ndege
Waziri Mbarawa alisema Serikali ina jumla ya viwanja vya ndege 58 vilivyo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kimoja kilicho chini ya KADCO.
Alisema kwa sasa Tanzania ina jumla ya ndege 12 za kisasa ambazo zinatoa huduma ndani na nje ya nchi, lakini taratibu za uingizaji wa ndege nyingine tano umekamilika, hivyo hadi kufikia mwaka 2023, kutakuwa na ndege 17 zitakazokuwa na uwezo wa kushindana na mashirika mengine ya ndani, kikanda na kimataifa.
Alisema bandari za Tanzania zimeendelea kuimarishwa kwa minajili ya kutoa huduma bora baada ya kuongezwa kina, jambo linalosababisha upakiaji na ushushaji wa mizigo kuwa rahisi.
Kwa upande mwingine, Profesa Mbarawa alikiri kuwapo kwa changamoto katika ujenzi wa barabara zake ambazo zinajengwa chini ya kiwango ikiwemo barabara ya Iringa- Dodoma ambayo ina muda mfupi lakini imeshaanza kuchakaa. Ili kukabiliana na jambo hilo,alisema wamenunua gari la kisasa ambalo linatumika kupima ubora wa barabara, hivyo kila wakati watakuwa wakipima barabara kabla ya kuipokea.