SERIKALI imeombwa kumchukua pundamilia anayeishi kambi ya wafugaji kwa mwaka mmoja sasa ili kuipunguzia familia hiyo tatizo la kugombana na wananchi wanaomtafuta mnyama huyo kwa ajili ya kitoweo.
Ombi hilo lilitolewa na wafugaji wa jamii ya Kisukuma wanaoishi na pundamilia huyo, walidai kitendo cha viongozi kukaa kimya na kuwaacha waendelee kuishi na mnyama hiyo kimewaweka kwenye matatizo na hofu kutokana na kuwapo kwa tishio kutoka kwa baadhi ya watu kumnyemelea ili wamfanye kitoweo.
Wakifafanua taarifa hiyo kwa nyakati tofauti, wanafamilia hao Emmanuel Matonange, Miru Matonange na Mawele Matonange, walisema pundamilia huyo alionekana akiwa amefuatana na punda wa kufugwa Desemba 2020.
Walisema siku zilizofuata waliondoka na mnyama huyo akiwa amefuata na kundi la punda wa kufugwa na ng’ombe na kwenda kumuacha kwenye pori, lakini kilicho washangaza kila walipofanya hivyo pundamilia huyo alifuata nyayo na kurudi kambini kwao.
Walisema baada ya jaribio hilo kushindikana walitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nampungu ili kuepuka mkono wa sheria wa kuwa na nyara ya serikali bila kibali.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nampungu, Mohammde Bwanali, alikiri kuwapo taarifa ya mnyama huyo katika kambi ya wafugaji na alipiga simu kwa ofisa wanyamapori wa wilaya hiyo na kumjulisha juu ya uwapo wa mnyama huyo.
Pia maofisa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere (TANAPA), walipigiwa simu kutaarifiwa hali iliyomfanya ajiridhishe kuwa sasa mnyama huyo angeondolewa katika maeneo hayo, lakini cha kushangaza waliwachukua na kuwapeleka polisi wafugaji hao na kumuacha mnyama huyo mikononi mwao.
Kaimu Ofisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Tunduru, Ombeni Simon Hingi, alisema tayari suala hilo wameliwasilisha ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwa ajili ya hatua za utekelezaji.
“Hatujajua ni kwanini mnyama huyo aliingia katika kundi hilo na kuanza kuishi kirafiki na wanyama wanaofugwa, hivyo ili kujua chanzo chake inafaa watafiti kutoa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwenda katika maeneo hayo na kufanya utafiti ili kujiridhisha na sababu ya tukio hilo,” alisisitiza Hingi.
Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Tunduru, Limbega Hassan, alisema kuwa taarifa zinaonyesha kuwa pundamilia hao walikuwa wawili, mmoja aliuawa na wananchi wa eneo hilo na wanahisiwa kutoka kwenye hifadhi ya jamii ya Chingoli au waliachwa na wenzao katika eneo la mapito ya ushoroba wa hifadhi za selous kwa upande wa Tanzania na Niasa kwa upande wa nchi jirani ya Msumbiji.
Alisema kwa sasa wanaendelea kufuatia nyendo za mnyama huyo kwa njia za kiintelijensia wakiwa wanashirikiana na uongozi wa serikali ya kijiji hicho hadi zoezi la kumwondoa mnyama huyo litakapokamilika