Rais Uhuru Kenyatta amemfuta kazi mkuu wa huduma ya magereza nchini Kenya Wycliffe Ogalo siku chache baada ya wafungwa watatu wanaotumikia kifungo kwa makosa yanayohusiana na ugaidi kutoroka katika gereza lenye ulinzi mkali
Badala yake Rais amemteuawa brigidia mstaafu John Kibao Warioba kuchukua mahala pake
katika taarifa iliotolewa na msemaji wa Ikulu ya rais Kanze Dena , Rais Kenyatta amesema nafasi ya Wycliffe Ogalo itachukuliwa mara moja "kuimarisha uwajibikaji katika safu ya uongozi wa vyombo vyote vya usalama".
Bw Kenyatta pia aliagiza mashirika ya usalama kutumia "rasilimali zote zilizopo" kuwasaka waliotoroka.
Waliotoroka ni pamoja na Mohamed Ali Abikar, ambaye alihukumiwa kwa jukumu lake katika shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa 2015 ambapo watu 148 waliuawa.
Mtu wa pili alikamatwa mwaka wa 2012 kutokana na shambulio lililozuiwa dhidi ya bunge la Kenya na wa tatu kwa kujaribu kujiunga na kundi la wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia.
Mamlaka pia imetoa wito kwa umma, kutoa taarifa kuhusu waliotoroka watatu na kutangaza zawadi ya shilingi milioni 20 za Kenya sawa na ($178,000; £132,000).