Dar es Salaam. Baada ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka minne kabla hajaachiwa hivi karibuni, hatimaye mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira ameanza harakati za kuzishtaki kampuni na taasisi za fedha anazozituhumu kuhusika katika wizi wa fedha za Serikali zilizomsababishia kesi ya uhujumu uchumi.
Katika kutimiza azma yake hiyo, Rugemalira amewasilisha maombi ya kibali cha kufungua na kuendesha mashtaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya kampuni na taasisi hizo kama mwendesha mashtaka binafsi.
Mfanyabiashara huyo aliyekaa ndani kwa miaka minne na miezi mitatu, ameachukua hatua hiyo ukiwa ni mwezi mmoja na nusu tangu alipatoka mahabusu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumfutia mashtaka yaliyokuwa yakimkabili yeye na wenzake watatu, Septemba 16.
Katika mchakato huo Rugemalira ambaye ni mmliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, amefungua maombi hayo dhidi ya watuhumiwa 11 zikiwamo taasisi za fedha na watu binafasi ambao anawatuhumu kuisababishia Serikali hasara ya Sh61 trilioni.
Maombi hayo tayari yamepangwa kusikilizwa mahakamani hapo Novemba 10 mwaka huu, na pande zote yaani waombaji (Rugemalira na kampuni yake ya VIP Engineering) na wajibu maombi wote wametakiwa kufika siku hiyo kwa ajili ya kuyasikiliza maombi hayo.
Wajibu maombi hao ambao Rugemalira anawatuhumu ni Benki ya Standard Chartered (Hong Kong), Benki ya Standard Chartered Tanzania, Benki ya Standard Chartered (Malaysia) Berhad, Wartsila Netherlands B.V na Wartsila Tanzania Limited.
Wengine ni Sanjay Rughani ambaye kwa sasa ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Samir Subbrwai ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered (Hong Kong), Abrar Anwai ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered (Malyasia) Berhad.
Vilevile wamo Bill Winters, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered na Hakan Agnevall ambaye ni Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wartsila Corporation.
Katika hati ya kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Rugemalira anayejitambulisha kama mshauri binafsi wa kimataifa wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na mwanahisa mkuu wa VIP Engineering and Marketin Limited, anaanza kwa kutoa historia ya sakata hilo.
Anadai mwaka 2005 baada ya IPTL kufunga shauri lililokuwa limeanza tangu Februari 25 mwaka 2002, Benki ya Standard Chartered (SCB) kupitia kampuni tanzu yake, Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) na Danaharta (SBCHK) walikusudia kuandaa mkataba wa makubaliano na, uuzaji na ununuzi wa IPTL.
Hata hivyo, Rugemalira anaituhumu Kampuni ya Mechmar ambayo ilikuwa mbia mkuu wa IPTL kula njama na SCB kukwepa kulipa dola 4.2 milioni za Marekani ambazo ni asilimia nne ya ushuru wa forodha katika mkopo wa IPTL wa dola 105 milioni wa Juni 28 mwaka 1997.
Rugemalira anadai katika kiapo chake kuwa kukwepa malipo hayo ni kosa la jinai chini ya Kifungu cha 73(2)(a) cha Sheria ya Ushuru wa Forodha iliyorekebishwa mwaka 2019.
Pamoja na makosa mengine aliyoyaainisha, Rugemalira anadai maombi hayo yanakusudia kurejesha Sh61 trilioni ambazo Standard Chartered Bank Group na washirika wake walifanya ulaghai kuchepusha fedha hizo kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na VIP Engineering isivyo halali.
Rugemalira na mwenzake Harbinder Singh Seth, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu Juni 19, mwaka 2017 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa na mashtaka 12 kabla ya kuongezwa aliyekuwa mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege.
Kesi hiyo ilitokana na kashfa ya uchotaji wa mabilioni ya pesa katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za uwekezaji kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopinga malipo hayo kuwa yalikuwa makubwa.
Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na pande hizo mbili kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo hayo kusubiri utatuzi wa mgogoro huo.
Mashtaka hayo yaliyokuwa yakimkabili Rugemalira na wenzake ni kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya dola 22,198,544.60 na zaidi ya Sh309.46 bilioni.
Hata hivyo, akiwa mahabusu, mara kadhaa Rugemalira alisisitiza kutokuwa na makosa huku akimtaka DPP amuondoe kwenye kesi hiyo ili amsaidia kuwapata wezi halisi wa fedha za Serikali kuwa fedha hizo zilizoibwa ni nyingi kuliko hizo zilizokuwa kwenye mashtaka yao ila maombi yake yahakuzingatiwa.