Rais wa Uganda, Yoweli Museveni (kushoto) akikabidhi mfano wa funguo yenye rangi ya bendera ya Uganda kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kulia) ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya shule ya msingi Museveni iliyojengwa wilayani Chato kwa ufadhiri wa serikali ya Uganda. Ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh3.9 bilioni. Picha na Mgongo Kaitira
Chato. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema wazo la ujenzi wa Shule ya Msingi Museven lilianza Julai 13, 2019 wakati wa ziara ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliyoifanya katika Wilaya ya Chato baada ya kualikwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dk John Magufuli.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano na ufunguzi wa shule hiyo, Profesa Ndalichako amsema wakati wa ziara hiyo, Rais Museven aliomba eneo ili aweze kujenga shule ya msingi wilayani humo kama zawadi kwa Watanzania.
“Kutokana na heshima kubwa na nia njema ya Rais Museven, Serikali ilitenga eneo lenye ukubwa wa ekari 11.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule hii,”amesema
Amesema eneo hilo limepimwa na kusajiliwa plot namba 51/block B nyamilezi ambapo ujenzi huo ulianza Februari 11, 2020 na kukamilika Februari 11 mwaka huu.