Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi Desemba 13, 2021 atakutana na madalali ili kuwekana sawa kwenye utendaji wao.
Waziri Lukuvi ametoa kauli hiyo leo Novemba 21, 2021 wakati akizungumzia miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Sekta ya Ardhi.
Hivi karibuni yaliibuka malumbano kwenye mitandao ya kijamii kufuatia agizo la Waziri Lukuvi kuhusu malipo mara mbili wanayochukua madalali wanapopeleka watu kupanga nyumba au kuuziana mali.
Amesema lengo lake ni jema kwa kukutana na watu hao Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwekana sawa kwa nia njema akisema madalali hawataondolewa kwani wana umuhimu.
"Kwanza sina nia ya kuwaondoa madalali kwa kuwa wana umuhimu wao katika kurahisisha kazi za watu, ndiyo maana nimewaita tuzungumze pamoja," amesema Lukuvi.
Amesema kuna baadhi ya madalali wamekuwa wakilipwa fedha nyingi kwa pande zote akitolea mfano wa hivi karibuni kuna mtu aliuza nyumba Sh80 milioni Jijini Dodoma lakini mwenye nyumba akalipwa Sh43 milioni.
Katika hatua nyingine Waziri amerudia kauli yake kuwa ni marufuku kwa mtu, taasisi au Serikali kuchukua ardhi ya mwananchi kwa matumizi yake kabla hajalipa fidia.
Amesema ulipaji fidia siyo hisani bali ni sheria inayomtaja anayetwaa ardhi lazima alipe fidia tena iwe stahiki kwa soko la wakati huo.