Shahidi Aibua Utata Kizimbani Kesi Kina Mbowe


Dar es Salaam. Utata uliibuka jana katika kesi ya uhujumu uchumi na ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu baada ya shahidi wa Jamhuri kukutwa na diary (shajara), simu na karatasi wakati akitoa ushahidi.


Hali hiyo ilisababisha sintofahamu mahakamani baada ya kiongozi wa mawakili wa utetezi, akiwamo Peter Kibatala kuomba Mahakama ifute ushahidi aliokwishautoa akidai alikuwa akisoma ‘visaidizi’ hivyo.


Shahidi huyo wa pili katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi dhidi ya kina Mbowe, DC Msemwa alikuwa akitoa ushahidi jana kuhusiana na maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohamed Ling’wenya ambayo mawakili wa utetezi wanataka yasipokewe mahakamani kama kielelezo katika kesi hiyo.


Wanadai alipewa tu maelezo yaliyokwisha andikwa katika Kituo cha Polisi Mbweni na kulazimishwa kusaini huku akitishiwa kwa bunduki kuwa mateso aliyoyapata Moshi yataendelea endapo hatasaini.


Soma zaidi:Mbowe katika muonekano tofauti mahakamani


Kibatala ndiye aliyeibua malalamiko ya shahidi huyo kuwa na diary, simu na kijikaratasi na kumwomba Jaji Joachim Tiganga kuvichukua na kuvihakiki na Mahakama imhesabu kuwa amekosa sifa za kuwa shahidi endapo itathibitishwa alikuwa ameandika.


ADVERTISEMENT

Kibatala: Mheshimiwa naona shahidi aliyepo mahakamani ana simu na diary (shajara) na ana karatasi, hivyo tunaomba ushahidi alioutoa akiwa chini ya kiapo uondolewe katika kumbukumbu za mahakama.


Jaji: Umeona hivyo vifaa anavyo?


Kibatala: Vifaa anavyo, tena mbele ya mabenchi mawili ya mawakili wa Serikali. Nimeona shahidi tangu zamani alikuwa emotional (mwenye mhemko) na alikuwa anaandika, hivyo akaguliwe.


Jaji: Unataka akaguliwe sasa hivi au tuache kwanza upande wa mashtaka wamalize kutoa hoja zao?


Kibataka: Hivyo vitu akabidhi kwa ofisa wa Mahakama halafu awe chini ya ulinzi kama tunaweza kufanya hivyo.


Jaji: Sawa.


Kufuatia madai hayo, shahidi huyo alikabidhi vifaa hivyo kwa karani wa Mahakama, na Jaji kutoa fursa kwa upande wa mashtaka kuendelea kutoa hoja zao za kupinga upande wa utetezi wanaotaka barua ya Naibu Msajili iliyotolewa na DC Msemwa kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo.


Baada ya pande zote kukamilisha uwasilishaji wa hoja, Kibatala aliiomba Mahakama ielekeze ‘diary’ ya shahidi huyo ihifadhiwe na Mahakama hadi pale itakapotoa uamuzi juu ya suala hilo, akidai shahidi huyo alikiuka kiapo chake.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando alifanya jitihada za kumlinda shahidi wao akiieleza Mahakama, “hatujasikia popote kuwa vitu anavyodaiwa kuandika vimetumiwa kutoa ushahidi. Hicho alichosema Kibatala tukianza kuingia kwenye zoezi hilo tunahitaji kuwa waangalifu. Simu ni kitu binafsi.”


Jaji Tiganga alitumia muda kidogo kumhoji Kibatala akitaka kujua kama shahidi huyo wa Jamhuri alikuwa akizitumia ‘diary’ na simu.


“Tukumbushane sheria. Kabla shahidi hajaingia kizimbani ni nini anachotakiwa kufanyiwa, upekuzi au kufanya nini. Nasema hivi ni vizuri kujiridhisha nikisema tuanze kupekua simu tunaangalia wapi. Kama ‘diary’ tunaweza kupekua lakini kwenye simu tutakuwa tunaenda mbali, tutakagua nini?” alihoji Jaji Tiganga


“Kwenye simu naona ugumu, arudishiwe, lakini weekend (mwisho wa juma) hii nendeni mkafanye research (utafiti) katika maeneo hayo halafu Jumatatu tutaona namna gani ya kufanya, ila simu arudishiwe na diary itabaki mahakamani.


Hata hivyo, Wakili Kibatala alishikilia msimamo wake akidai kuwa aliarifiwa mapema na Joseph Haule (Profesa J) kuwa shahidi huyo alikuwa akisoma, hasa wakati akitaja majina ya askari na alikuwa na kalamu wakati hoja za kisheria zikiendelea kuhusiana na pingamizi linalobishaniwa.


Baada ya vuta nikuvute, Jaji Tiganga aliamuru ‘diary’ inayobishaniwa ibaki mahakamani na shahidi arudishiwe simu yake, akieleza ugumu wa kuamua suala hilo. Pia, alizitaka pande zote katika kesi hiyo kufanya utafiti wa nini sheria inasema pale inapotokea hali kama hiyo.


“Naona kuna vifungu vya sheria vimetajwa lakini kafanyeni utafiti Jumatatu mkija tuangalie linafanywa kwa sheria ipi,” alisema Jaji Tiganga.


Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi ilipangwa kuanza kusikilizwa saa nne asubuhi, lakini ilichelewa kwa zaidi ya saa mbili na nusu kwa sababu ambazo hazikuelezwa.


Upande wa mashtaka walimleta shahidi DC Msemwa ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hiyo ndogo ili athibitishe kuwa mshtakiwa Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenywa walifikisha na kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam baada ya kukamatwa Moshi.


Upande wa utetezi wanapinga maelezo ya onyo ya Ling’wenya yasipokewe mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri, wakidai mshtakiwa huyo alilazimishwa kusaini maelezo hayo huku akiwa ameshikiwa silaha.


Wanadai kuwa mteja wao hakuwahi kuandika maelezo ya onyo katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.


Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan na Adam Kasekwa, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka sita, ikiwemo kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.


Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Pius Hilla ambaye ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Msemwa (31) aliyekuwa akifanya kazi Kituo cha Polisi Oysterbay, alidai Agosti, 2020 alikuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam katika kitengo cha General Duties (majukumu ya jumla).


Ifuatayo ni sehemu ya ushahidi wake jana:-


“Agosti 7, 2020 niliingia kazini alfajiri na nilikuwa Central (Kituo Kikuu cha Polis Dar es Salaam). Nilikuwa zamu katika chumba cha mashtaka.


“Siku hiyo majira ya asubuhi watu wa kwanza kufika alikuwa afande Kingai, Jumanne na askari wengine wawili wakiwa wameshika bunduki wakiwa na watuhumiwa wawili.


Kwa wakati ule, afande Kingai alikuwa RPC (Mkuu wa Polisi wa Mkoa) Arusha na afande Jumanne alikuwa anatoka Makao Makuu.


“Kingai, Jumanne na wenzake walifika chumba cha mashtaka. Afande Jumanne aliuliza ‘nani anahusika hapa chumba cha mashtaka?’ Nilijibu ‘ni mimi.’


“Alinikabidhi watuhumiwa, kumbukumbu namba na aina ya kesi inayowakabili. Aliniambia wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kutenda makosa ya ugaidi.


“Baada ya kuwapekua watuhumiwa niliwapeleka chumba cha mahabusu pale Central Polisi, Dar es Salaam. Pia, niliandika majina yao katika kitabu cha kumbukumbu za mahabusu.


“Baada ya Kingai na wenzake kuniletea watuhumiwa wale sikujua waliondoka kwenda wapi. Watuhumiwa walioletwa pale CR ni Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya.


“Baada ya kuwapokea na kuwaingiza maabusu, haukupita muda mrefu afande Kingai alikuja na kumchukua mtuhumiwa aitwaye Adam Kasekwa kwa ajili ya kwenda kuandika maelezo.


“Baada ya afande Kingai kuja kumchukua Kasekwa, naye afande Jumanne alikuja na kuniambia nimtolee mtuhumiwa Mohamed Ling’wenya kwa ajili ya kwenda kuandika maelezo ya onyo. Afande Kingai alimchukua Kasekwa hadi ofisi ya juu kwa RCO.


“Baada ya watuhumiwa kutolewa mahabusu na kwenda kuandika maelezo walirejeshwa pale CR na kisha nikawapeleka mahabusu.


“Watuhumiwa wanapotolewa kwenda kuhojiwa huwa tunaingiza taarifa zao katika kitabu cha kumbukumbu na kuwahoji afya zao, hivyo hivyo wakimaliza kuhojiwa lazima tujaze tena katika kitabu cha DR na kisha kuwaingiza maabusu,” alidai Msemwa.


Kesi hiyo itaendelea Jumatatu Novemba 15, 2021

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad