Shahidi Kesi ya Ole Sabaya Aanika Alivyoidhinisha Tsh mil 90




SHAHIDI wa tisa katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, amedai aliidhinisha mfanyabiashara, Francis Mroso atoe Sh milioni 90 kwa mkupuo. Shahidi huyo, Mary Mayoka (40) ni Meneja wa benki ya CRDB tawi la Kwa Mrombo, jijini Arusha.

 

Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Tasilia Asenga, shahidi huyo alidai alimhoji mfanyabiashara huyo kwa nini alitaka kutoa fedha hizo kwa wakati mmoja na alimjibu kuwa alitaka kumlipa mtu aliyefuatana naye benki hapo.

 

“Nilimfuata yule kijana (mlipwaji) kuzungumza naye kumuuliza kama ana akaunti benki na alinijibu kwamba hana na nilimshauri afungue akaunti lakini alikataa alitaka kulipwa fedha taslimu na alisema angekuja siku nyingine kufungua akaunti,” alidai shahidi huyo.

 

Mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda, Mayoka alidai amekuwa Meneja wa tawi CRDB la Mwa Mrombo tangu Januari mwaka jana.

 

Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashitaka matano likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

 

Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha(29) na Nathan Msuya (31).

 

Mayoka alidai kuwa, benki hiyo imeweka utaratibu wa kulinda fedha za wateja kwa kuwa na mifumo imara ya ulinzi zikiwamo kamera za CCTV zenye kuhifadhi picha za video ndani ya mwaka mmoja.

 

Shahidi huyo alidai kwamba Januari 22, mwaka huu, saa 11 jioni, alifika ofisini kwa Mhasibu wa benki ya CRDB kumweleza kuwa Mroso anataka kutoa fedha nyingi hivyo alitaka kwenda kuzungumza naye kama meneja wa tawi hilo.

 

Alidai mhasibu alimuuliza Mrosso alitaka kutoa shilingi ngapi na alimweleza kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kutoau Sh milioni 90.

 

Aliieleza mahakama hiyo kuwa, baada ya mteja kutaka kulipwa fedha taslimu, akiwa meneja wa tawi alitoa ruhusa fedha hizo kutolewa na walipatiwa na kuwekewa kwenye boksi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad