Shahidi kesi ya Sabaya aieleza mahakama alivyotoa Sh90 milioni




Mfanyabiashara Francis Mrosso (44) anayedaiwa kuombwa rushwa ya Sh 90 milioni na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, ameanza kutoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, akidai kuwa alitishiwa asipotoa fedha hizo atafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.


Leo Novemba 22, 2021 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Patricia Kisinda, Mrosso ambaye ni mmiliki wa gereji ya kutengeneza magari ya Mrosso Injector Pump na fundi magari, ameanza kutoa ushahidi wake wa msingi akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas.



Katika kesi hiyo Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano wanayodaiwa kuyatenda Januari 22, 2021 jijini Arusha.



Shahidi huyo ameieleza Mahakamana namna Sabaya na vijana wake walimtishia na kumtaka awapatie Sh90 milioni ambazo alidai kumpatia moja ya vijana hao wa Sabaya baada ya kuzitoa benki ya CRDB tawi la Kwa Mromboo jijini Arusha.



Mrosso amedai kuwa Sabaya na wenzake walimtishia kuwa anakwepa kodi ya Serikali kwa kuingiza spea za magari kwa njia ya panya huku akimtishia kuwa atafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana.



Amedai kuwa alipata woga baada ya kuelezwa maneno hayo ambapo pia alilazimika kutoa fedha hizo kwa sababu Sabaya alimweleza aispotoa wataondoka naye.



Hakimu anayesikiliza kesi hiyo ameiahirisha hadi kesho Novemba 23, 2021 ambapo Mrosso ataendelea kutoa ushahidi wake wa msingi kabla ya kuanza kuhojiwa na mawakili wa utetezi.



Katika kesi hiyo watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad