Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema serikali yake itaziondoa sheria tata za mashamba ambazo zilisababisha maandamano yaliyodumu kwa mwaka mmoja kutoka kwa maelfu ya wakulima waliosema sheria hizo zitaharibu riziki yao.
Modi ametoa tangazo hilo la kushtukiza wakati wa hotuba ya televisheni iliyorushwa moja kwa moja. Amesema mchakato wa kikatiba wa kuondoa sheria hizo utaanza Disemba wakati bunge litaanza vikao vyake vya msimu wa baridi.
Sheria hizo zilipitishwa Septemba mwaka jana na serikali ikazitetea, ikisema zilikuwa muhimu kuimarisha sekta ya kilimo ya India na itaongeza uzalishaji kupitia uwekezaji wa kibinafsi.
Tangazo hilo limetolewa mnamo siku ya tamasha la Guru Purab, ambapo ni sherehe ya siku ya kuzaliwa ya muasisi wa dini ya makalasinga Guru Nanak, na kabla ya uchaguzi muhimu katika majimbo kama Uttar Pradesh na Punjab. Wengi wa waandamanaji walikuwa wakulima wa Kikalasinga na Punjab.
OPEN IN BROWSER