Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palagamba Kabudi amesema Serikali imepanga kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Rufani kwa kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kuhusu umri wa kuolewa.
Profesa Kabudi alisema hayo Novemba 18,2021 alipoeleza mafanikio ya wizara yake katika miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.
Muswada huo alisema umepelekwa kamati ya Bunge kwa ajili ya kuupitia lakini iliurejesha serikalini ikitaka kuendelea kwa mashauriano na wadau.
Alisema wanaendelea kuwashirikisha wadau wengine kuona namna nzuri ya kutekeleza mahitaji ya watu ya umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18.
Kuhusu uwakilishi wa mawakili, Profesa Kabudi alisema mahakama zote za mwanzo zenye mahakimu wenye shahada ya sheria mawakili wanaruhusiwa katika mashauri yao.
Alisema ndani ya mwaka mmoja mahakama za mwanzo zote nchini zitakuwa na mahakimu wenye shahada ili mawakili waweze kutumika.
Kuhusu kutafsiri sheria ziwe kwa Kiswahili, Profesa Kabudi alisema hadi sasa Sheria 154 zimetafsiriwa katika rasimu ya awali na mchakatochuo unaendelea kwa miaka miwili.
“Tunatumia rasimu ya kwanza ili sheria hizi zitumike baada ya hapo tukibaini maeneo yanayohitaji marekebisho tutafanya. Jambo kubwa ni kuwa na istilahi za kisheria kwa lugha ya Kiswahili,” alisema.
Maandamano na mikutano ya kisiasa
“Maandamano na mikutano ya kisiasa haijazuiwa nchini ila inaratibiwa na imewekewa utaratibu. Ndio maana ninasema haijazuiwa. Hakuna jambo linalofanyika bila utaratibu. Tunasoma sura ya pili ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano kuhusu haki za binadamu bila kusoma ibara ya 30 iliyoweka mipaka ya wewe kufaidi uhuru wako,” alisema
Alitaja mipaka iliyowekwa kuwa ni mtu kutoingilia uhuru na haki ya mwingine, maagizo ya umma, usalama na afya.
Waziri huyo alisema mipaka hiyo imewekwa pia katika uhuru wa kuabudu na imani ambapo mtu anatakiwa kuifuata anapotumia uhuru wake.
Alisema hakuna uhuru usio na mipaka ambao kuepusha ghasia kwa watu wengine na mipaka hiyo haipo Tanzania pekee bali mataifa mengine pia.
Alisema Tanzania ni nchi pekee Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye Sheria ya Vyama vya Siasa baada ya kurejea katika mfumo wa vyama vingi ambayo imeweka wajibu na majukumu huku vihakikishiwa ruzuku kwa vile vinavyoshinda ubunge na udiwani inayotokana na kodi za wananchi.
Kuhusu maandamano, alisema lazima kuwe na utaratibu ikiwamo kujulikana kwa mahali na siku ya kuyafanya.
Alisema kuna nchi zimeweka utaratibu maandamano ni Jumamosi tu ili siku za wiki watumishi wafanye kazi na kwa nchi za Ulaya maandamano yanafanyika nje ya mji.
Kuhusu utaratibu wa kufuatwa ili kuandamana, alisema Sheria ya Usalama Barabarani imeweka mwongozo.
“Ukiisoma vyema hata magari ya harusi yakizidi 10 inabidi ukaombe ruhusa trafiki kwamba leo mimi mtoto wangu atakuwa anaoa nitakuwa na magari kama 20 hivi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu utaratibu wa makubaliano ya awali (plea bargain) unachochea watu kufanya makosa, Profesa Kabudi alisema Tanzania si nchi ya kwanza kuuanzisha na umekuwa ukitumika kwa miaka mingi Marekani na Uingereza. Alisema makubaliano hayo yana viwango, kanuni na utaratibu wake.