Uongozi wa Klabu ya Yanga unayo haki ya kupunguziwa lawama na kuongezewa pongezi kwa namna walivyoufanya usajili hasa wa msimu huu.
Yale makosa ya kuleta wachezaji wa kawaida wa kigeni angalau msimu unaoendelea yanaonekana kupungua sana. Wastaarab wanaoipenda Yanga wanayo maongezi chanya na ya haki kuliko wapiga kelele wanaotokwa mapovu ya kinazi.
Aliyemleta Khalid Aucho alijua anafanya nini na kwa wakati gani. Kaleta kiungo aliyekuja Tanzania kufanya kazi anayoijua vyema. Aucho anazo sifa zote za mlinzi anayesimama mbele ya mabeki wawili wa kati.
Aliyemleta Mayele anajua lilikuwa wapi tatizo la msingi la timu na akaja na suluhisho la uhakika. Mayele ni aina ya wafungaji wanaopoteza nafasi moja na akaitumia nyingine kwa umahiri wa hali ya juu.
Moloko kule kushoto pembeni ni winga msumbufu anayetumia akili. Na uwepo wa Shaban Djuma unaongeza uzoefu kutokea pembeni. Wakongomani sita kila mmoja wao ni mchezaji chuma.
Yanga imebadilika kabisa. Imejaa wachezaji wazoefu wenye kuweza kuamua mechi ndani ya dakika yoyote ile.
Ikiwa na kocha Mtunisia Nabi, Yanga inacheza mpira wa kimataifa na hata wachezaji wazalendo wanajikuta wakilazimika kupandisha viwango vyao.
Feisal Salum anakuwa kiungo mtamu kila dakika anayozungukwa na wachezaji wa kigeni walioingiza uzoefu kwenye timu.
Simba wanajikuta ghafla tu wakilazimika kukaza kamba za viatu vyao na kucheza mpira mkubwa zaidi.
Visingizio vya kusema mlango waliolazimishwa kuutumia ni sababu ya timu yao kupata sare tasa dhidi ya Coastal Union ni matokeo ya presha wanayoipata wanapoitazama Yanga inayocheza kwa maarifa na malengo. Wajikite kuimarisha kikosi chao kuliko kujifariji kwa maneno yasiyo na uhakika wala ushahidi.
Mdhamini alipoamua kuongeza pesa kwa kila timu alilenga zaidi kuimarisha ushindani. Simba watambue kuwa huwezi kucheza mpira ukiwa unakariri yaleyale ya miaka iliyopita.
Watafute makocha wa viwango vya juu na watulize akili. Kwa ufupi waiwazie zaidi timu yao ina upungufu upi na unaweza kufanyiwa kazi namna ipi kuliko kuwashika uchawi Yanga.