SIMBA imeamua kumuondoa katika hoteli ya kisasa, kocha msaidizi wa timu hiyo, Mnyarwanda, Thierry Hitimana, na kumpangia nyumba ya kisasa iliyopo Mbezi Makonde jijini Dar, katika eneo ambalo wanaishi watu wenye hadhi.
Hitimana ameondolewa kwenye hoteli hiyo ambayo amekuwa akiishi kwa muda mrefu huku kocha mpya,
Mhispania, Pablo Franco naye akiwa amepangiwa apatimenti ya kisasa iliyopo Mbezi Beach.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Ijumaa limezipata, uongozi wa timu hiyo umeamua kurudisha mtindo wa zamani kwa kuwapa nyumba za kuishi makocha wa timu hiyo badala ya kuwa na maisha ya kwenye mahoteli.
Simba imekuwa na kawaida ya makocha wake kuishi katika hoteli ya Sea Scape ambapo alianzia Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Didier Gomes pamoja na Hitimana ambaye kwa sasa amepewa nyumba.
Championi lilimtafuta Hitimana ambaye amekiri kuondoka kwenye hoteli hiyo baada ya kupewa nyumba na uongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kuishi. “Sasa hivi sipo hapo hotelini, nimepewa nyumba ya kuishi maeneo ya Mbezi Makonde ndiyo nilipo, hata mwalimu mkuu hayupo, naye amepewa apartments maeneo hayahaya ya Mbezi ila sijui sehemu gani,” alisema Hitimana.
Stori na Ibrahim Mussa, Dar es Salaam