Deo Kanda na Papy Tshishimbi wamesaini kandarasi ya kuitumikia Kitayosce kutoka mkoani Tabora inayoshiriki Championship.
Kitayosce inashiriki Ligi hiyo kwa msimu wa pili, ambapo mabosi wa timu hiyo wameanza kuisuka upya kuhakikisha msimu ujao wanaungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga.
Mkurugenzi wa timu hiyo, Yusuph Kitumbo, amethibitisha nyota hao kumalizana nao na siku yoyote kuanzia leo watawasili nchini kuungana na hiyo iliyoweka kambi wilayani Misungwi mkoani Mwanza kuendelea na mazoezi na wenzao.
"Tayari Tshishimbi ameshasaini na leo (jana), Kanda amesaini na wote watatua kuungana na wenzao huko Misungwi Mwanza, tumeamua kuwaleta mapema kukamilisha kila kitu haraka kwani hata Ligi ikisimama kambi itaendelea" amesema Kitumbo.
Tshishimbi raia wa DR Congo, aliwahi kukipiga Yanga akiwa Nahodha wa timu hiyo kabla ya kutemwa msimu uliopita, sawa na Kanda aliyetemwa Simba na sasa wawili hao wanarejea tena nchini.
Kitayosce inakuwa timu ya pili kwenye Championship kuwa na wachezaji wa kigeni, ikiungana na DTB yenye nyota kadhaa kama Amis Twambe, Tafazwa Kutinyu na Nicolous Gyan.