Mahakama Kuu Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo inatarajiwa kutoa uamuzi utakaomaliza mvutano wa mawakili kuhusiana na upokewaji wa kielelezo cha upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Mbowe na wenzake hao, Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya wanakabiliwa na kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga.
Pingamizi hilo dhidi ya kitabu cha kumbukumbu ya mahabusu kutoka Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, likitaka kisipokelewe mahakamani hapo kama ushahidi, lilikuja baada ya kuwasilishwa na shahidi Koplo Mpelelezi Ricardo Msemwa.
Msemwa ambaye kituo chake ni Oysterbay, aliwasilisha kitabu hicho Jumatano iliyopita katika Mahakama hiyo wakati akitoa ushahidi wake.
Mawakili wa utetezi, waliweka pingamizi hilo wakati shahidi huyo akitoa ushahidi katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshitakiwa, Mohamed Ling’wenya yasipokewe wakidai hakuyatoa akiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam wala Kituo cha Polisi Mbweni jijini humo.
Jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Peter Kibatala akisaidiana na Jeremiah Mtobesya, lilitoa hoja tatu katika pingamizi hilo, likidai kitabu hicho kilikwishatolewa uamuzi katika kesi kama hiyo ya Adam Kasekwa, lakini utaratibu haukufuatwa kukipata, na Mahakama haijatoa amri ya kitabu hicho kutoka.