Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akizungumza na Wakili wake Mosses Mahuna katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakati kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake sita ilipokuwa inasikilizwa. Picha na Janeth Mushi
Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeonyeshwa video ya matukio yanayodaiwa kutokea benki ya CRDB Arusha, tawi la Kwa Moromboo Januari 22 mwaka huu.
Video hizo zimeonyeshwa leo Novemba Mosi, 2021 mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka huu, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.
Video hizo zimeonyeshwa mahakamani hapo na shahidi wa nane wa Jamhuri ambaye ni ofisa uchunguzi wa Maabara ya Uchunguzi wa Kielektroniki kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Johnson Kisaka.
Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Jamhuri, Felix Kwetukia shahidi huyo alionyesha video hizo kupitia projekta, ambapo picha za wateja katika benki hiyo wakiingia na kutoka kupata huduma.
Katika video mojawapo inaonyesha watu watatu wakishuka kwenye gari linaloonekana kuwa na rangi ya bluu majira ya saa 10:10 alasiri, ambapo mmoja alikuwa amevalia koti la bluu lililofika magotini, huku mwingine akiwa amevalia kaunda suti ya bluu na wa tatu akiwa amevalia tshirt ya mistari na kofia nyeusi.
Watu hao walionekana kupitia video hiyo wakiingia benki hiyo ambapo baada ya aliyekuwa amevaa koti la bluu kuingia na kuchukua karatasi ya benki (bank slip) kisha kuelekea kwenye dirisha la huduma (teller), huku kijana huyo akiwa nyuma yake ambapo muda mwingi alionekana kuwa karibu na mtu huyo kila anapoenda ndani ya benki hiyo.
Katika video hizo zilizoonyesha kuanzia nje ya benki hiyo hadi ndani, ilianzia saa 10:09 alasiri hadi saa 11:05, jioni ambapo watu wawili aliyekuwa na kofia na mwenye koti walitoka nje ya benki hiyo wakiwa wamebeba fedha katika boksi moja kubwa.
Awali kabla hawajatoka nje ya benki hiyo fedha hizo zilitolewa na mmoja wa maafisa wa benki zikiwa juu ya kiti kilichokuwa na magurudumu kabla ya kuziweka ndani ya boksi hilo kisha kusaidiana kubeba kutoka nje ya benki hiyo.
Baada ya watu hao wawili kutoka fedha hizo ziliwekwa siti ya mbele huku aliyekuwa amevaa koti la bluu akipanda upande wa dereva na aliyekuwa amevalia fulana na kofia akipanda siti ya nyuma ya dereva ambapo mtu wa tatu waliyekuwa naye aliondoka mapema ndani kisha akaonekana nje ya benki hiyo akiwa anaongea na simu.
Baada ya shahidi huyo kumaliza kuonyesha video hizo Wakili Kwetukia aliieleza mahakama kuwa shahidi amemaliza kutoa ushahidi wake wa msingi.
Katika kesi hiyo watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano la kwanza ni kudaiwa Januari 22,mwaka huu ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.
Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh 90 milioni matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro.
Hakimu Kisinda ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Mawakili wa utetezi watakapoanza kumhoji shahidi huyo.