KATIKA kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Bunge limeitaka serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za kukodi ndege, ili shirika hilo liweze kukua na kujiendesha kwa faida.
Limesema mkataba wa ukodishaji wa ndege ulioingiwa kati ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na ATCL unaitaka ATCL kuanza kulipa gharama za kukodi ndege baada ya kukabidhiwa ndege, hata kama ndege hizo hazijaanza kufanya safari zake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti, Sillo Baran, aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2022/23, pamoja na mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23.
Alisema hatua hiyo iende sambamba na uwezekano wa kusamehe ada ya pango la ndege walau kwa miaka miwili kipindi ambapo athari za ugonjwa wa corona zilikuwa kubwa kati ya mwaka 2019/20 na 2020/21.
Mbali na hilo, Baran alisema serikali inapaswa kukamilisha haraka ujenzi wa viwanja vya ndege vya mikoa, ili kuongeza mtandao na idadi ya miruko ya ndege ya shirika hilo ndani ya nchi.
Alisema pia, serikali inapaswa kulipa madeni yaliyokuwa ya shirika hilo kabla ya kufufuliwa, ili kusafisha vitabu vya shirika.
Kadhalika, alisema katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/22 serikali ilitumia Sh. billioni 557.8 katika kuimarisha usafiri wa anga na ATCL.
Baran alisema kamati ilipata fursa ya kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi na kubaini changamoto ambazo zinakwamisha shirika hilo kusimama imara na kupunguza hasara.
“Kwanza kutokana na athari za ugonjwa wa corona shirika liliathirika, lakini hakukuwa na mpango wowote wa serikali kulinusuru shirika hilo kama yalivyo mashirika mengine ya ndege duniani, badala yake Wakala wa Ndege za Serikali aliendelea kutoza gharama ya pango kwa ndege zote hata zile zilizopaki kwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 1.5 kwa mwezi,” alisema Baran na kuongeza:
“Aidha, Wakala wa Ndege za Serikali inaitaka ATCL kuweka amana ya matengenezo ya ndege yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.2 kila mwezi wakati matengenezo ya ndege yanafanywa na ATCL wenyewe na si wakala wa ndege za serikali”.
Alisema pia kamati ilibaini kwamba mkataba wa ukodishaji wa ndege kati ya TGFA na ATCL unaitaka ATCL kuanza kulipa gharama za kukodi ndege mara tu baada ya kukabidhiwa ndege hata kama ndege hizo hazijaanza kufanya safari zake.
Baran alisema kamati pia ilibaini kwamba kasi ya kukamilisha viwanja vya ndege vya mikoa ni ndogo kuliko kasi ya kununua ndege.
Alisema pia kamati ilibaini kwamba asilimia 86.4 ya madeni yote ya ATCL mdai ni serikali.