Wadaiwa sugu NHC kuanza kufurumushwa kesho




Wadaiwa sugu NHC kuanza kufurumushwa kesho
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kuanza kuwaondoa wapangaji wa nyumba zake ambao ni wadaiwa sugu kuanzia kesho. 

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula wakati akizungumza na wapangaji wa shirika hilo jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa Dk Mabula, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linadai wapangaji wake takribani Sh bilioni 26 jambo alilolieleza linachangia kuzorotesha kasi ya utendaji kazi wa shughuli za kila siku za shirika ikiwemo ukarabati wa nyumba hizo. 

"Tutakachofanya sasa, yeyote aliyelimbikiza deni na tumeshampa notisi lakini bado halipi kodi basi zoezi la kumuondoa litafanyika bila hata kumtaarifu upya," alisema Dk Mabula. 


 
Aliongeza kuwa, oparesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu wa nyumba za NHC itaenda sambamba na kuwaondoa wapangaji wote wasio waaminifu waliopangisha nyumba za shirika kwa gharama nafuu huku nao wakipangisha watu wengine kwa gharama kubwa. 

Aliwahakikishia wapangaji wa nyumba za NHC kuwa, Shirika hilo limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake ikiwa ni mpango wake wa miaka mitano na tayari kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 50 kimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi mbali na kupongeza shughuli zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa, aliliomba shirika hilo kuona namna ya kuzifanyia marekebisho baadhi ya nyumba zake hasa upakaji upya wa rangi baada ya Serikali kuwapanga upya wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga maeneo ya miji ili kupendezesha mji. 


Naye Meneja wa NHC Mkoa wa Mwanza, Fadhili Anyegile alisema kwa mwaka 2021/2022  shirika hilo limeweka mikakati ya kuhakikisha linapunguza malimbikizo ya madeni ya wapangaji kwa asilimia mia moja, kutoa elimu kwa wapangaji juu utaratibu wa kulipa kodi kwa wakati na kuendelea na zoezi la kufanya matengenezo makubwa na madogo katika nyumba zake ili kuzifanya kuendelea kuwa imara. 

Wakati huo Dk Mabula  amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza kero na migogoro ya ardhi nchini kwa kutatua iliyopo na kuweka mikakati ya kuzuia migogoro mipya ikiwemo utwaaji maeneo ya wananchi bila kulipa fidia. 

Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kutatua migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyopo Wilaya ya Nyamagana ukiwemo mgogoro wa wananchi na mwekezaji kampuni ya Pamba Engineering uliopo Kata ya Mhandu. 

Mgogoro mwingine ni baina ya Msimamizi wa Mirathi Ndugu Abuu mwana familia ya Marehemu Mzee Seif eneo la Miembeni Mtaa wa Nera Kata ya Isamilo kuhusu umilikishwaji eneo lao la urithi na ulipwaji fidia kwa wananchi wa mtaa wa Kisoko Kata ya Luchelele kutokana na Serikali kutwaa eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad