Wafungwa hatari watoroka gereza la Kamiti Kenya, Msako mkali wafanyika



Wasimamizi saba wa magereza wamekamatwa nchini Kenya baada ya wanamgambo watatu wa Kiislamu wanaotajwa kuwa hatari kutoroka katika gereza lenye ulinzi mkali nje kidogo ya mji mkuu, Nairobi.



Waliotoroka ni pamoja na Mohamed Ali Abikar, ambaye alihukumiwa kwa kuhusika kwake katika shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa mnamo 2015 ambapo watu 148 waliuawa.

Mamlaka imelaumu ulegevu na uzembe uliosababisha kutoroka kwa wafungwa hao.

Msako wa nchi nzima unaohusisha mashirika kadhaa ya usalama unaendelea.

Mamlaka pia imetoa wito kwa umma, kutoa shilingi milioni 20 za Kenya ($178,000; £132,000) kwa atakayetoa taarifa kuhusu watu hao watatu, ambao wote wamekuwa jela kwa makosa yanayohusiana na ugaidi.

Mtu wa pili alikamatwa mwaka wa 2012 kutokana na shambulio lililodhibitiwa kwenye bunge la Kenya na wa tatu kwa kujaribu kujiunga na kundi la wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia.

Katika taarifa, Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i alisema sababu rasmi iliyotolewa na mamlaka katika gereza la Kamiti lenye ulinzi mkali kuhusu madai ya kutoroka Jumatatu haikuongezea chochote.

“Tutafanya msako mkali kuwatafuta watu hawa watatu. Ni wahalifu hatari na lazima tuwapate,” alisema.

“Tutachukua hatua thabiti kuhakikisha uzembe wa aina hii hautokei tena,” aliongeza.

Gereza la Kamiti
Aliongeza kuwa kuna uwezekano wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka zaidi baada ya uchunguzi wa polisi kukamilisha kazi yake.

Ali Abikar alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 41 jela katika gereza la Kamiti, baada ya kuhukumiwa mwaka wa 2019 na wengine watatu kwa kuhusika katika shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa kaskazini-mashariki mwa Kenya.

Mapema tarehe 2 Aprili 2015, washambuliaji waliokuwa na silaha nzito walivamia chuo kikuu na kuwapiga risasi walinzi wawili kabla ya kuwafyatulia risasi wanafunzi, baadhi yao waliokuwa wakijiandaa kwa mitihani.

Walioshuhudia walisema Wakristo walitengwa na wanamgambo hao na kupigwa risasi.

Watu hao wanne wenye silaha waliuawa katika eneo la tukio na mtu aliyepanga shambulizi hilo, Mohamed Kuno, aliuawa katika uvamizi nchini Somalia mwaka 2016.

Hilo lilikuwa shambulio la pili baya zaidi nchini Kenya.

Shambulio la al-Qaeda katika ubalozi wa Marekani mwaka 1998 liliua zaidi ya watu 200.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad