MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, wamesema kwenye kata zao kumetokea mkanganyiko wa ujenzi wa vyumba vya madarasa baada ya fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuelekezwa kwenye miradi mipya na si iliyokuwa ikiendelea.
Walibainisha hayo kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Walitaka kufahamu vigezo vilivyotumika mpaka fedha zilizotoka kwa rais zisiendeleze kwenye miradi ya ujenzi wa vyumba vilivyoanza kujengwa kwa nguvu ya halmashauri, wadau na wananchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Missana Kwangura, walipokea mgawo wa zaidi ya Sh bilioni 7.7 ambazo kati ya miradi inayotakiwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa 94 katika shule za sekondari na maboma 54 kwenye shule za msingi shikizi.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Diwani wa Kata ya Madibira, Juma Msiminyungu alisema halmashauri kwa kushirikiana na wadau ilikwishaanza juhudi za kujenga vyumba vya madarasa katika shule za sekondari zilizokuwa na uhitaji na yapo maeneo ujenzi ulifikia hatua nzuri.
Msiminyungu alisema baada ya kusikia Rais anatoa fedha, ujenzi ulisimama, wadau wakijua zitamalizia kazi zilizobaki na kukamilisha ujenzi wa majengo husika.
Alisema sasa wanashindwa kuelewa iwapo fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi mingine mipya.
Diwani wa Kata ya Ihahi, Bahati Salumu alisema kupitia michango ya wananchi na wadau baadhi ya kata majengo yalikwishafikia hatua ambayo ni kazi ya halmashauri kumalizia kama ilivyokuwa makubaliano ya awali.
Alisema wananchi hawataielewa serikali watakapoona majengo yao yanabaki katika hatua iliyofikiwa. Alisema hali hiyo inawapa wakati mgumu maofisa watendaji waliopita kwa wananchi na wadau wengine kukusanya michango kwa ajili ya ujenzi wa awali ambao sasa utasimama na kuanza ujenzi mwingine mpya.
"Tunawapa wakati mgumu sana watendaji wetu wa vijiji na kata. Hawa ndio walipita kukusanya michango tena maeneo mengine kwa kutumia nguvu kidogo. Lakini pia kuna baadhi ya shule ilikuwa tukijenga vyumba hivyo uhitaji unakwisha sasa tunapokwenda kuanza ujenzi wa jengo jipya la pili lile la kwanza litabaki la kazi gani," alihoji Salumu.
Akitoa maelezo ya fedha hizo, Mkurugenzi Kwangura alisema maelekezo ya fedha za rais ni ya kutoka ngazi za juu na wala hayakufanyika kwenye ngazi ya mkoa wala wilaya. Alisema ni wakati wa kutekeleza maagizo badala ya kutupiana lawama.
"Fedha zimetolewa nchi nzima na maelekezo ya serikali ni kujenga hivyo ni maelekezo ya juu na wala si uamuzi wa mtu wa kati. Maelekezo ya majengo yaliyokuwa yanaendelea kujengwa ni kwamba yataombewa fedha kama miradi viporo ikiambatanishwa na picha zake na fedha zake zitaletwa kwa maelekezo yake," alisema.
Alifafanua zaidi: "Na fedha hizi zinaingizwa kwenye akaunti ya shule husika au eneo husika la mradi. Kwa upande wa shule shikizi kwa kuwa zenyewe zinakuwa hazina akaunti fedha zake zitaingizwa kwenye akaunti za shule mama za msingi kwa kuwa ndizo zilizozizalisha. Lakini pia wakati ujenzi huu unaendelea ushiriki wa wananchi pia ni muhimu," alisisitiza.