Wapinzani wa Simba kwenye kombe la Shirikisho, Red Arrows wameanza vibaya kwenye ligi kuu ya Zambia baada ya kucheza michezo 7 na kuvuna alama 8, ambapo matokeo hayo hayatoi taswira yoyote kuelekea mechi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, ambao bado wanatafuta ubora wao kwenye ligi kuu ya NBC.
Novemba 28, Simba itaanzia nyumbani katika mchezo wa kwanza na timu hizo zitarudiana Lusaka Zambia katika Uwanja wa Mashujaa, Desemba 5, mwaka huu.
Timu itakayopata matokeo mazuri katika mechi mbili baina ya timu hizo, itatinga hatua ya makundi ambayo itashirikisha jumla ya timu 16 zitakazogawanywa katika makundi manne.
Hizi ni baadhi ya taarifa muhimu za Red Arrows itakayoumana na Simba katika hatua hiyo ya mwisho ya mchujo na inakuletea dondoo muhimu zinazoihusu.
Red Arrows ilianzishwa katika makao makuu ya Zambia, Lusaka mwaka 1978 na kuanzia hapo hadi sasa iko chini ya umiliki wa Jeshi la Anga la Zambia.
Katika mashindano ya ndani imekuwa ikitumia Uwanja wa Nkoloma unaoingiza mashabiki wasiozidi 7,500 lakini mechi zake za kimataifa imekuwa ikitumia Uwanja wa Mashujaa uliopo jijini Lusaka unaokidhi vigezo vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Red Arrow imetwaa mara moja taji la Ligi Kuu ya Zambia na pia imechukua Kombe moja la Zambia. Imetwaa pia taji moja la Chalenji na pia imetwaa Ngao ya Jamii huko Zambia mara moja
Katika mashindano ya kimataifa, Red Arrows imekuwa sio tishio sana kwani haijawahi kufuzu angalau hatua ya makundi tangu ilipoanzishwa na mara zote tatu za nyuma ilizowahi kushiriki mwaka 2005, 2009 na 2012 iliishia katika hatua za mtoano.
Mwaka 2005 iliiwakilisha Zambia katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuishia raundi ya pili, miaka minne baadaye ikaishia katika hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na mwaka 2012 ilikomea raundi ya awali.
Kitendo cha kufikia hatua ya mwisho ya mchujo ya Kombe la Shirikiso Afrika katika msimu huu ambayo watakutana na Simba ndio mafanikio makubwa hadi sasa ambayo wamewahi kuyapata kimataifa.
Timu hiyo imekuwa ikitumia jezi nyekundu kwa mechi zake za nyumbani na jezi zenye rangi ya bluu mpauko kwa mechi zake za ugenini na pia wana jezi nyeupe ambayo ni ya tatu.
Red Arrows walipata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita nyuma ya Zesco United iliyotwaa ubingwa na Zanaco iliyomaliza nafasi ya pili.
Katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika walipangwa kukutana na Young Buffaloes ya Eswatini na katika mechi ya kwanza nyumbani, Zambia waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na wakatoka sare ya bila kufungana ugenini.
Raundi iliyopita walikutana na Primiero de Agosto ya Angola na walianzia nyumbani wakapata ushindi wa bao 1-0 na mechi ya marudiano ugenini wakalazimisha sare tasa.
Kikosi cha Red Arrows kinanolewa na Kocha Oswald Mutapa ambaye ni Raia wa Zambia.
Kina wachezaji watano wa kigeni ambao ni kipa Yasin Mugabi kutoka Uganda,mabeki Elvis Bissong (Cameroon) na Trésor Yamba Yamba (DR Congo), kiungo Alassane Diarra (Mali) na mshambuliaji Alidor Kayembe (Congo).
Wengine waliobakia ni Wazambia ambao ni makipa Charles Kalumba na Kenny Mumba wakati mabeki ni Benedict Chepeshi, Prosper Chiluya, Chiteta Kwalombota, Nickson Mubili, Allan Kapila, Joseph Lungu na Edward Tembo.
Viungo ni Felix Bulaya, Leonard Mulenga, Francis Simwanza, George Simbayambaya na Saddam Phiri wakati washambuliaji ni Rick Banda, Hope Katwishi, Joseph Phiri, James Chamanga na Chrispine Chakulanda.