Siku moja baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kutangaza kuwavua uanachama viongozi wake saba, wenyewe wamesema wao bado ni wanachama halali.
Pia wamesema wanakusudia kupeleka malalamiko yao kwa msajili wa vyama vya siasa.
Viongozi hao saba ni miongoni mwa 14 waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kula njama za kukihujumu chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 10, 2021 Mkurugenzi wa zamani wa habari na Uenezi, Abdul Kambaya amesema maamuzi yaliyotolewa na chama hicho ni batili na hayajafata Katiba ya chama.
Alisema wanaomshauri Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho, Ibrahimu Lipumba ni watu ambao hawana weledi kwenye masuala ya kisiasa.
“Sisi hatukati rufaa, kwasababu kwa mujibu wa mabadiliko tuliyoyafanya mwaka 2019 ni kwamba mkutano mkuu uakaat kila baada ya miaka mitano, kwahiyo siamini kama chama kitakubali kuingia gharama kubwa kuitisha kikao cha dharura kujadili jambo hili. Hivyo uamuzi wetu ni kwenda kupeleka malalamiko yetu kwa msajili na kupata ufafanuzi wa vifungu vya katiba ambavyo vimekiukwa,” amesema Kambaya.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu, Hamis Mohamed Faki amesema wako tayari kukaa meza moja kujadili hilo lakini kama itashindikana wataendeleza mapambano kuhakikisha wanaipeperusha bendera ya chama hicho.
“Hatutakubali, hatutayumba hata siku moja, CUF ni mama. Hivyo tuungane kwa pamoja kuhakikisha chama chetu kinaendelea kuwa imara na haki zinafuatwa,” amesema Faki.
Aliyekuwa Mbunge wa Mchinga (CUF), na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho, Hamidu Bobali amesema kitendo kilichofanyika ni kukiukwa kwa makusudi matakwa ibara ya 11(6)ya katiba ya chama inayotaka mtuhumiwa kupewa haki ya kujitetea.
Pia amesema chama kimepuuza kwa makusudi matakwa ya ibara ya 115 (1) ya katiba ya chama ambayo inayoweka masharti ya uhalali na maamuzi ya kura zinazopigwa, ni lazima ziwe zimezidi nusu ya wajumbe waliohudhuria.
“Pia imekiukwa ibara ya 81 ya chama chetu ambayo inataja wajumbe halali wa Baraza Kuu. Wapo ambao walishiriki kupiga kura ndani ya kikao cha Baraza kuu ambao kwa mujibu wa katiba ya chama sio wajumbe halali bali ni waalikwa tu.
“Mimi sijafukuzwa ila nimepewa onyo kali. Hivyo silitambui karipio nililopewa na ninaungana na hawa wenzangu kwamba maamuzi haya ni batili, sifukuziki kwa mtindo huu na sitoki abadani,” amesisitiza.
Mbali na Kambaya, wengine waliofukuzwa ni Hamida Abdallah Huweishi aliyekuwa mgombea mwenza wa Profesa Ibrahimu Lipumba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Chande Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya Vijana ya CUF (JUVICUF), Ali Makame Issa, Mtumwa Ambari Abdallah , Mohamed Vuai Makame na Dhifaa Bakari ambao wote ni wajumbe wa Baraza Kuu la CUF.