NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ amezua mjadala kwa mashabiki wa Fenerbahce huko Uturuki kwa kile ambacho anakifanya kwenye michuano ya Europa Ligi akiwa na Royal Antwerp ya Ubelgiji.
Hakuna ambaye anaonekana kuamini kuwa huyu ndiye yule yule ambaye alikuwa kwenye kikosi chao na kushindwa kuonyesha makali yake.
Mjadala wa Samatta uliibuliwa na mashabiki wa timu hiyo kwenye mitandao ya kijamii, mara baada ya mshambuliaji huyo kuisaidia Royal Antwerp kupata pointi moja ugenini huku Fenerbahce ikikumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Olympiacos Piraeus.
Uwanja wa komenti wa Instagram kwenye posti mbalimbali za klabu hiyo ndilo eneo ambalo mashabiki hao walitumia kueleza hisia zao.
Mr Erdal alimtaka kocha wa timu hiyo, Vitor Pereira kubwaga manyanga kutokana na kitendo cha kuwaachia wachezaji ambao kama wataunda kikosi chao wanaweza kuwa tishio kuliko wachezaji waliosalia klabuni hapo kwani si lolote.
“Hatuwezi kufika kwa staili hii, hivi kweli sisi wa kushindwa hata kupata nafasi ya kwenda hatua inayofuata?Hii ni aibu. Hapakuwa na sababu ya kuwachia wachezaji ambao wangeweza kuwa msaada katika hatua hii, “ alisema.
Nurdin Hafidhi alisema,”Haya ndio mavuno ya kile ambacho tulipanda, hatukuwa na sababu za kumwachia Samatta, tulipaswa kumpa muda kama ambavyo imekuwa kwa Ozil.”
Ndani ya michezo mitano ya Europa Ligi msimu huu, Samatta ametupia mabao matatu na kumfanya kufikisha jumla ya mabao 16 huku akiwa na asisti mbili kwenye michuano hiyo tangu aanze kucheza kwa mara ya kwanza, 2016 akiwa na KRC Genk.
Royal Antwerp anayoichezea Samatta ipo kundi D na Fenerbahce, wote wamepoteza nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo, kundi lao linaongozwa na Frankfurt wenye pointi 11, wakifuatiwa na Olympiacos wenye pointi tisa.