Vurugu mitaani zimeutikisa tena mji mkuu wa Sudan, Khartoum leo Alhamisi siku moja baada ya vikosi vya usalama kuwaua kwa kuwapiga risasi waandamanaji wapatao 15.
Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji wengi wanaopinga mapinduzi ya kijeshi kaskazini mwa Khartoum usiku kucha kuamkia leo. Msako huo mkali umelaaniwa na kimataifa.
Polisi walibomoa vizuizi vya muda vilivyowekwa na waandamanaji siku iliyotangulia. Walioshuhudia wamesema baadaye mchana waandamanaji walirudi barabarani na kujenga upya vizuizi hivyo ambapo polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya ili harakati za kusafisha barabara ziendelee lakini waandamanaji walijibu kwa kuwarushia polisi mawe.
Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa watu Kujumuika Clement Voule, amesema amepokea ripoti za kutisha za kuongezeka kwa matumizi ya nguvu ya kijeshi dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani.
Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuweka shinikizo kwa utawala wa Sudan uache mara moja ukandamizaji wa raia na uheshimu haki za binadamu.