Watu kadhaa wamefariki dunia katika ajali iliyotokea kwenye Mto Congo, baada ya meli mbili kugongana uso kwa uso siku ya Jumatano, Novemba 17 usiku. Vyanzo vya usalama kutoka N'sele na serikali ya mkoa vinabaini kwamba watu kadhaa hawajulikani waliko, bila kutoka maelezo zaidi.
Kulingana na vyanzo hivi, Meli iitwayo Sanza na Moi na nyingine iitwayo Emmanuel, ziligongana mwendo wa saa tatu usiku, katika eneo la Mambutuka, kwenye Mto Congo, si mbali na makutano kati ya Mto Kasai na Mto Congo.
Watu wachache walionusurika wamefika mjini Kinshasa, kulingana na mjumbe wa serikali ya mkoa ambaye alihojiwa na Radio Okapi nchini humo.
Zoezi la utafutaji wa abiria waliokosekana linaendelea na kukusanya habari ili kujua kilichotokea.