Hospitali ya Chuo Kikuu cha Osaka nchini Japan imetangaza kuwa Watu katika eneo hilo (Wafanyakazi na Wagonjwa) wamekuwa wakitumia maji yanayotoka chooni kwa kunywa, kupikia na matumizi mengine kwa bahati mbaya bila kujua kutokana na mfumo wa kuunganisha mabomba kukosewa.
Taarifa iliyotolewa na Hospitali hiyo imesema imebaini kuwa bomba la maji safi lilipitishwa chooni kwa bahati mbaya na maji yanayotoka chooni yakawa yanachanganyika na yale safi na kutumiwa na Watu, hilo limebainika hivi karibuni wakati wakiwa wanatengeneza mfumo mpya wa kutibu maji .
Chuo hicho kimesema kinachunguza kujua chanzo cha uzembe huo lakini vipimo vya ubora wa maji vimeonesha hayana vijidudu vibaya vya kusababisha magonjwa na mpaka sasa hakuna aliyewahi kuugua kwa kutumia ya maji hayo huku wakisema huenda kutibiwa kwa maji hayo kumesaidia.
Uchunguzi wa awali umeonesha huenda mifumo na makosa hayo yalifanywa mwaka 1993 wakati Hospitali ikiwa inaanzishwa na endapo ni kweli basi huenda Watu wametumia maji hayo kwa zaidi ya miaka 25.