Waziri Mkuu Abiy aliapa Jumatano kuwazika maadui wa serikali yake na "damu yetu", wakati akiadhmisha kuanza kwa vita katika mkoa wa Tigray mwaka mmoja uliopita. Maadhimisho hayo yamefanyika huku TPLF ikiutishia mji mkuu.
Mshindi huyo wa tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2019, alikuwa akizungumza siku moja baada ya serikali kutangaza hali ya hatari nchini Ethiopia, na wakati vikosi vya Tigray vikitishia kusonga mbele kuelekea mji mkuu Addis Ababa.
"Shimo linalochimbwa litakuwa na kina kirefu, humo ndipo atazikwa adui na siyo ambapo Ethiopia inagawanyika," alisema Abiy katika hotuba wakati wa tukio kwenye makao makuu ya jeshi mjini Addis Ababa.
Waziri Mkuu huyo ambaye alishinda tuzo ya Nobel kwa kutatua mzozo wa muda mrefu na Eritrea, alisema "tutamzika adui yetu na damu yetu na mifupa na kuipandisha juu tena heshima ya Ethiopia."
Abiy Ahmed alishinda tuzo ya amani ya Nobel kwa kutatua mzozo wa muda mrefu na Eritrea.
Miito ya kufanya majadiliano kuepusha vita
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba akizungumza na Abiy siku ya Jumatano akimtaka kuiruhusu ofisi yake kuweka mazingira ya majadiliano ili kusitisha mapigano.
Wito wa awali wa kuwazika madui uliokuwemo kwenye taarifa iliyochapishwa na ukurasa rasmi wa Abiy kwenye mtandao wa Facebook mwishoni mwa wiki, uliondolewa na jukwaa hilo kwa kukiuka sera zake dhidi ya uchochezi na kuunga mkono vurugu, ilisema kampuni hiyo.
Wakati wa maadhimisho ya Jumatano ya mwaka mmoja wa mzozo huo, kulishuhudiwa ukimya na hafla ya kuwasha mishumaa kuwakumbuka wlaiouawa Novemba 3, 2020, wakati vikosi tiifu kwa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF - wakiwemo baadhi ya wanajeshi - walipoteka kambi za kijeshi mkoani Tigray.
Kufutia tukio hilo, Abiy alituma wanajeshi katika mkoa huo wa kaskazini.
Soma pia: Wakaazi wa Addis Ababa watakiwa kusajili silaha zao
TPLF iliongoza muungano tawala wa Ethiopia kwa takribani miaka 30 lakini ilipoteza udhibiti baada ya Abiy kuingia madarakani mwaka 2018 kufuatia maandamano makubwa ya kuipinga serikali.
Uhusiano na TPLF ulivurugika baada ya chama hicho kumtuhumu kujilimbikizia madaraka kwa gharama ya mikoa ya Ethiopia, tuhuma ambazo Abiy anazikanusha.
Mzozo huo katika taifa la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, umesababisha vifo vya maelfu ya watu, kuwalaazimisha milioni mbili kuyapa kisogo makazi yao, na kuwaacha watu 400,000 mkoani Tigray wakikabiliwa na njaa.
Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na Umoja wa Mataifa na tume ya haki za binadamu ya Ethiopia, ambao ripoti yake ilichapishwa jana Jumatano, ulionesha kuwa pande mbili zinazopigana zimetekeleza ukiukaji unaoweza kuwa uhalifu wa kivita.
Umoja wa Afrika umesema jana kuwa mwenyekiti wake Moussa Faki Mahamat, alikuwa akifuatilia mzozo nchini Ethiopia kwa wasiwasi mkubwa, na kuzihimiza pande mbili kufanya majadiliano.
Jirani wa Ethiopia Kenya imeongeza ulinzi kwenye mpaka wake.
Will Davison, mchambuzi mwandamizi katika shirila linalofuatilia mizozo duniani ICG, alisema mafanikio ya vikosi vya Watigray yameongeza shinikizo dhidi ya serikali ya Abiy.
"Hivi sasa, inaonekana vigumu kwa muungano wa shirikisho kuzuwia vikosi vya Tigray, na baadhi ya viongozi wake wamesema hivi karibuni kwamba katika hatua hii ya mwisho hawatazamii kujadiliana na Abiy," alisema.
Vikosi vya Tigray hivi sasa viko katika mji wa Kemise mkoani Amhara, kilomita 325 kutoka mji mkuu, alisema msemaji wa TPLF Gatachew Reda, akiahidi kupunguza vifo katika kampeni yao ya kuitwaa Addis Ababa.
"Hatuna nia ya kuwafyatulia risasi raia na hatutaki umuagaji damu. Ikiwezekana tungependa mchakato uwe wa amani," alisema.
Mtaalamu wa kikanda anaewasiliana na pande zinazopigana na aliezungumza na sharti la kutotajwa jina, alisema TPLF huenda ikajizuwia kusonga mbele kuelekea Addis Ababa hadi itakapochukuwa udhibiti wa barabara kuu inayotoka nchi jirani ya Djibouti kuelekea mji mkuu.
Hilo linahitaji kuukamata mji wa Mille. Gatachew alisema siku ya Jumanne kwamba vikosi vya Tigray vilikuwa vinaukaribia mji huo.
Serikali ya Abiy imetangaza hali ya hatari ya miezi sita siku ya Jumatatu, ambayo inawaruhusu raia waliotimiza umri wa kuhudumu jeshini kupatiwa mafunzo na kukubali majukumu ya kijeshi.
Wakazi wawili wa Addis Ababa walisema wataitikia wito wa Abiy wa kujiunga na jeshi kupambana dhidi ya vikosi vya Tigray.
"Sote tunataka kuwa na nchi, hivyo sote tunapaswa kuitikia wito," alisema Merkeb Shiferaw, mhandisi mwenye umri wa miaka 28.