WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuuboresha Mji wa Dodoma kwa kujenga miundombinu ya barabara, maji pamoja na nyumba za watumishi.
Amesema hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa shilingi bilioni 20 ambazo ni mkopo nafuu kwa Shirika la Nyumba la Taifa ili ziwe mtaji wa kujenga nyumba 1,000 katika maeneo ya Chamwino na Iyumbu jijini Dodoma ambao hadi kukamilika kwake mradi huo utagharimu Shilingi Bilioni 71 huku awamu ya kwanza ikitumia Bilioni 21.4 kukamilisha nyumba 404.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya ujenzi wa majengo ya Ofisi na Makazi kwa Watumishi wa Umma ili kupunguza gharama kubwa ya kodi ya pango pamoja na kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi hao katika kuwahudumia Watanzania.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Oktoba 31, 2021) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 1000 za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Chamwino na Iyumbu Mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa kukaa pamoja na DUWASA, TARURA na TANESCO ili kuona namna bora ya kushirikiana na kufanikisha upatikanaji wa miundombinu hiyo muhimu na kupunguza mzigo wa gharama kwa Shirika hilo ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kwa gharama nafuu.
“Wakurugenzi wa Halmashauri hususan halmashauri mpya tumieni Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na Watumishi Housing ili muweze kuharakisha ujenzi wa nyumba bora za watumishi wa Halmashauri kwa gharama nafuu.”
Aidha Mheshimiwa Majaliwa ameliagiza Shirika hilo kupunguza gharama za manunuzi kwa kununua vifaa kama mabati, mabomba, vigae kutoka kwa wazarishaji wa ndani ya nchi kwa kuweka oda maalum ili miradi ikamilike kwa muda uliopangwa na kuhakikisha sheria na taratibiu za manunuzi zinafuatwa.
Awali, akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa nyumba 100 katika eneo la Chamwino Waziri Mkuu ameipongeza Wizara ya Ardhi pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa kwa hatua ya ujenzi nyumba hizo pamoja na mpango wa ujenzi wa nyumba za makazi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza wafanyakazi wakitanzania walioshiriki katika ujenzi wa nyumba hizo ikiwa ni utekelezaji wa msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikishwaji wa watanzania katika ujenzi wa miradi mikubwa ya ujenzi.
Kwa Upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi, amesema Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa haitaruhusu utaratibu wa mtu mmoja kununua nyumba nyingi katika eneo hilo na kisha kuanza utaratibu wa kupangisha, ila watatoa fursa sawa kwa Watanzania wa kada zote ili waweze kunufaika na mradi huo.
Nae Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt. Maulid Banyani pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutoa mkopo nafuu kwa Shirika hilo amesema awamu ya kwanza ya mradi wa nyumba 1000 unaotekelezwa na Shirika hilo Mkoani Dodoma ulianza Januari 6, 2021 kwa Iyumbu na Chamwino ulianza Februari 1, 2021.
“Mradi huu mkubwa unaohusisha ujenzi wa nyumba za makazi 1000 katika Jiji la Dodoma utagharimu Shilingi bilioni 71 hadi kukamilika ambapo awamu hii ya kwanza yenye nyumba 404 itagharimu shilingi bilioni 21.4 na kazi kubwa ya ujenzi itakuwa imekalika ifikapo Desemba 2021 na kubakiwa na ukamilishaji wa kazi chache za nje ambazo nazo zitaisha mwezi Januari 2022.”