KUELEKEA katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa leo Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, Yanga na Ruvu Shooting zimetambiana vikali.
Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema wachezaji wa timu yao wamekubaliana kuzipata pointi tatu dhidi ya Ruvu Shooting ili kuendelea kuongoza ligi ikiwa ni sehemu ya kuyakimbilia mafanikio yao.
Nao Ruvu Shooting, wamefunguka kuwa, watatibua rekodi ya Yanga ya kutofungwa wala kutoa sare msimu huu katika ligi hiyo.Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Msaidizi wa Ruvu Shooting, Rajab Mohamed, alisema: “Tunamshukuru Mungu tupo vizuri, tumejiandaa vizuri kuvunja rekodi ya Yanga msimu huu.
“Hatuna majeruhi kwenye kikosi chetu, wachezaji wote wapo sawa, kikubwa ni kupata matokeo kwenye mchezo huo wa kesho (leo).“
Tunajua kuwa Yanga hawajawahi kupoteza mchezo wowote msimu huu, ila sisi tutakuwa wa kwanza kwani tumeona michezo yao minne waliyocheza na tumeona madhaifu yao, hivyo tutapata ushindi.”
Kabla ya mechi moja ya jana kati ya Mbeya Kwanza dhidi ya Polisi Tanzania, Yanga ilikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda mechi zote nne ilizocheza.