MWINYI Zahera, aliyekuwa kocha msaidizi ndani ya Timu ya Taifa ya DR Congo, amesema matokeo ya mchezo wa leo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars dhidi ya DR Congo, ni 50/50 kutokana na hesabu za timu zote mbili.
Mchezo huo uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, umekuja baada ya ule wa kwanza uliochezwa DR Congo timu hizo kufungana bao 1-1.
Akizungumza na Spoti Xtra, Zahera ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Timu za Vijana ndani ya Yanga, alisema hakuna mwenye uhakika wa ushindi wa mchezo huo wa leo kwa asilimia 100 zaidi ya kila timu
kuwa na asilimia 50.
“Mchezo wa kwanza walipokutana, timu ya DR Congo iliwachukulia kawaida Taifa Stars na wachezaji ambao
walikuwa wanajulikana ni wachache akiwemo Mbwana Samatta, walikuwa wanajua wachezaji wengi wa Taifa
Stars ni wa ndani, lakini kwa kuwa walishacheza nao watakuja kwa mtindo tofauti.
“DR Congo wanajua kwamba ili wasonge mbele lazima washinde, wakifungwa wanatoka katika mbio za kuwania
kufuzu Kombe la Dunia.
“Kwa upande wa Taifa Stars nao wanahitaji kushinda ili kusonga mbele, hapo unaona namna gani mchezo
utakuwa mgumu kwa timu zote mbili.
“Naweza kusema hata kama Stars watakuwa nyumbani, haimaanishi kwamba watashinda kwa wepesi, ni moja ya
mchezo mzuri kwa kuwa unazikutanisha timu ambazo zinasaka ushindi,” alisema Zahera.
NA LUNYAMADZO MLYUKA NA HAWA ABOUBAKHARI