Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)
BAADA ya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukosa idadi kubwa ya wabunge wa upinzani, Chama cha ACT-Wazalendo, kinatarajia kuzindua mbinu za kuisimamia Serikali hususan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, nje ya mhimili huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 25 Desemba 2021 na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Taarifa ya Zitto imesema kuwa, mbinu hizo zitazinduliwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho, utakaofanyika tarehe 29 Januari 2022.
Zitto ameandika, ACT-Wazalendo imeamua kuifuatilia miradi ya maendeleo ya Serikali, ili kuhakikisha fedha za umma pamoja na za mkopo kutoka Benki ya Dunia (W.B) na Shirika la Fedha Duniani (IMF), zinazotumika zinaakisi thamani ya miradi husika.
“Kati ya Mwezi Machi na Desemba 2021, Benki ya Dunia imeidhinisha fedha kwa Tanzania jumla ya Dola za Marekani 2.3 bilioni, katika sekta mbalimbali. Sekta ya elimu ikiongoza kwa dola 1.43 bilioni,” ameandika Zitto.
Kati ya Mwezi Machi na Desemba 2021 Benki ya Dunia imeidhinisha Fedha kwa Tanzania Jumla ya USD 2.3 Bilioni katika sekta mbalimbali. Sekta ya Elimu ikiongoza kwa USD 1.43B. Ufadhili huo ni;
-Tanzania ya Kidigitali $150M
-Elimu ya Juu $425M
-Barabara Jumuifu $300M
1/2
— Zitto MwamiRuyagwa Kabwe (@zittokabwe) December 25, 2021
Mwanasiasa huyo ameandika “bila ya Bunge madhubuti usimamizi wa fedha hizi na hata zile za IMF utakuwa mbovu. Sisi @ACTwazalendo tumeamua kufuatilia kila mradi na kuibua aina yeyote ya ubadhirifu.”
“Tunazindua mbinu mpya za kuisimamia Serikali nje ya Bunge kwenye Mkutano Mkuu Maalumu mwisho wa Januari 2022,” amesema Zitto.
Bunge hilo la 12 limebeba wabunge wengi wa Chama Tawala Cha Mapinduzi (CCM), ambao wako zaidi ya 320 huku vyama vya upinzani vikiambulia wabunge 25, wa majimbo watano (ACT-Wazalendo 4, Chadema 1) na viti maalum wasio na chama bungeni 19.
Idadi hiyo ya wabunge inatokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo yalikipa ushindi wa zaidi ya asilimia 90 CCM.
Pia, taarifa ya Zitto imesema ACT-Wazalendo kitazindua mkakati mpya wa siasa ili kuimarisha demokraisa uwajibaki na kuchochea mabadiliko.
Mbali na uzinduzi wa mikakati hiyo, taarifa ya Zitto imesema mkutano huo mkuu maalum wa ACT-Wazalendo, utatumika kumchagua Mwenyekiti wa chama hicho, ili kuziba pengo lililoachwa na Maalim Seif Shariff Hamad, aliyefariki dunia tarehe 17 Februari 2021.