ACT-Wazalendo yawachongea wateule wa Rais




Ado Shaibu, Katibu Mkuu 
CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemuomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya viongozi wa umma, wakiwemo wateule wa Rais, ili kuwachukulia hatua wanaokiuka misingi ya utendaji kazi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, tarehe 27 Desemba 2021 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ACT-Wazalendo, Janeth Rithe, wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, katika ziara yake kwenye Jimbo la Tunduru Kaskazini, mkoani Ruvuma.

“ Ado amemtaka Waziri Mchengerwa kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha viongozi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na misingi ya utawala bora, kwa sababu baadhi ya wakuu wa wilaya na watendaji wengine, wanatumia sana ubabe na vitisho, badala ya kuongozwa na ubunifu, maarifa na ushirikishwaji,” imesema taarifa ya Rithe.

Katika taarifa hiyo, Ado alidai, kuna baadhi ya viongozi wa umma akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, wanakiuka maadili ya kazi kwa kutumia madaraka yao vibaya, ikiwemo kuwalazimisha wakulima wilayani humo kutoa fedha kwa ajili michango mbalimbali.


 

Julius Mtatiro, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru
“Nimekwenda Tunduru Kusini na leo (jana) nipo Tunduru Kaskazini. Kote nimeelezwa kilio cha wananchi juu ya Mtatiro. Si sahihi kwa mkuu wa wilaya kuwa ubabe, kukata fedha za wakulima wa Korosho kuchangia timu ya mpira bila kushirikisha wanachama wa Vyama vya Ushirika (AMCOS),” alidai Ado na kuongeza:

“Sio sawa pia kwa mkuu wa wilaya kuingilia uendeshaji wa ushirika na kuwalazimisha wananchi kuuza mazao kwa bei ya chini. Nimeelezwa kwenye kijiji Cha Tulieni, Kata ya Nakapanya, wananchi walipigwa mabomu kwa sababu ya kutafuta bei nzuri ya mbaazi wilaya ya jirani. Masuala haya yangeweza kushughulikiwa kwa njia shirikishi, sio kwa mabomu.”

MwanaHALISI Online imemtafuta Mtatiro kwa njia ya simu, ili kupata ufafanuzi dhidi ya tuhuma hizo, ambaye amejibu kwa msisitizo kuwa hajibu propaganda.


“Sijibu propaganda mimi, sijibu propaganda,” amejibu Mtatiro.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad