ACT Wazalendo yawageuka Chadema, NCCR Mageuzi



Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT Wazalendo
LICHA ya baadhi ya vyama vikuu vya upinzani nchini kutangaza kususia kikao cha wadau wa tasnia ya siasa kupitia Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kuwa kitashiriki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na NCCR Mageuzi vimetangaza kutoshiriki mkutano huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 15-17 Desemba, 2021 Jijini Dodoma.

Viongozi wa vyama hivyo, John Mnyika Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi kwa upande wa Bara, Anthony Komu wamesema vyama vyao havitoshiriki mkutano huo kwa kuwa mapendekezo waliyowasilisha kwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, Juma Ali Khatibu hayakuzingatiwa.

Mapendekezo hayo ni pamoja na serikali kutoa tangazo la kusitisha zuio haramu la mikutano ya hadhara na shughuli nyingine za kisiasa kwa mujibu wa sheria na kanuni.


 
Wakati Chadema na NCCR Mageuzi wakionesha msimamo huo, taarifa iliyotolewa leo tarehe 14 Disemba, 2021 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ACT Wazalendo, Janeth Rithe, imesema Kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe ataongoza viongozi wenziwe kushiriki kikao hicho.


Janeth Rite, Naibu katibu mwenezi wa ACT-Wazalendo
Zitto ataambatana na Kaimu Mwenyekiti wa Chama Taifa, Dorothy Semu; Katibu Mkuu, Ado Shaibu na Mwanasheria Mkuu wa Chama, Omary Said Shaaban ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Taarifa hiyo imesema Msajili wa Vyama vya Siasa alipotangaza kikao cha Wadau wa Tasnia ya Siasa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), tarehe 24 Septemba 2021, ACT Wazalendi kiliweka bayana kutoshiriki kikao hicho kwa hoja tatu.


“Kwanza IGP si Msimamizi wa kisera wa tasnia ya kisiasa nchini, pili kutokuwepo kikaoni kwa Mawaziri wenye dhamana ya siasa nchini na tatu kugongana kwa ratiba baina ya kikao hicho na Mkutano wa Kitaifa wa Haki, Amani na Maridhiano ulioitishwa na Kituo Cha Demokrasia Tanzania.

Ilisema ACT Wazalendo watashiriki kikao hicho wakitambua kuwa katika miaka sita iliyopita, demokrasia imekandamizwa na kuvurugwa sana nchini.

“Tunakwenda kwenye kikao kama jukwaa la kusukuma mabadiliko ya uendeshaji wa siasa nchini.

“Ajenda zetu kuu kwenye kikao hiki ni; Mabadiliko ya Kikatiba na Kisheria kuhakikisha kwamba chaguzi nchini zinakuwa huru, za haki na zenye kuaminika na kuandikwa upya kwa Sheria ya Vyama vya Siasa ili kuhakikisha Vyama vyote vya Siasa nchini vinafanya shughuli zake kwa uhuru na usawa.


 
“Ajenda nyingine ni maboresho ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili vifanye kazi zake kwa weledi, haki na uhuru na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aachiwe huru kwa sababu kesi dhidi yake haina maslahi kwa umma,” ilisema taarifa hiyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad