MAKOCHA Pablo Franco wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga, mbinu zao zinanogesha Ligi Kuu Bara, kutokana na ukongwe wa timu wanazozifundisha kuwa mfano.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema tangu Nabi aanze kuifundisha timu, imekuwa ikimiliki mpira na baadhi ya wachezaji kupitia falsafa yake viwango vyao vimekuwa juu kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Shomari Kibwana.
Alisema kitendo cha Yanga kucheza pasi nyingi na kumiliki mipira, Nabi akitumia viungo wengi, timu inakuwa inajiamini na kujiondoa kwenye presha. “Nabi amejitafsiri ni muumini wa timu kuchezea mpira na kuumiliki ni kitu kizuri na timu inakuwa salama zaidi wanapokutana na timu shindani, pia naona kambadilisha Kibwana kutoka kulia hadi beki ya kushoto na anafanya makubwa,” alisema.
Kwa upande wa Pablo alisema ni mtaalamu wa soka lenye malengo, timu iwe imecheza vizuri au vibaya ana uwezo wa kupata alama tatu, kutokana na namna anavyowatumia wachezaji wake, kulinda timu kuwa salama.
“Nimeona anavyomtumia Benard Morrison kutafuta mipira yenye malengo ya kufunga, ndio maana Simba imekuwa na mabadiliko ndani ya muda mfupi, timu inaweza ikafanya lolote muda wote, hicho ni kitu kinacholeta chachu ligi kuu,”alisema.
Kauli yake iliungwa mkono na kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes aliyesema makocha hao wanaonyesha ukomavu wa ukongwe wa klabu wanazozifundisha, kujua kuwatumia wachezaji wao.
“Yanga ilianza vizuri ligi na ndio ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kushinda dabi hiyo, lakini Pablo ameonyesha mbinu kali ambazo zimeirejesha timu kwenye ushindani kwa muda mfupi, akisaidiana na Thiery Hitimana, kuhakikisha wanacheza kwa malengo wakati wanaendelea kutengeneza kikosi chao,”alisema na akaongeza kuwa;
“Nabi kupitia dabi kikosi chake kilicheza kwa maelekezo zaidi, hakutaka kujiachia jambo ambalo lingeweza kumgharimu, ila falsafa yake ni ya kumiliki mpira, hilo linaleta chachu ya ushindani kwenye ligi kuu,”alisema.
Mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma alisema; “Nimeona kikosi cha Simba kimekuwa na mabadiliko kwa muda mfupi, Pablo mbinu zake zitakuwa na ushindani mkali kadri muda unavyokwenda, soka lake ni la malengo zaidi, Nabi yeye soka lake timu inacheza pasi nyingi na kumiliki mpira, hicho ni kitu kizuri kwao.” Yanga inauwinda ubingwa na Simba wanapambana kuutetea kwa maranyingine na kuweka rekodi.