Moshi/Karagwe. Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza ametaja habari nane alizoziita ni mbaya za kutisha na zisizo na furaha zilizoikumba Tanzania mwaka 2021.
Moja ya habari hizo ni kuondokewa na Rais John Pombe Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17 katika hospitali ya Mzena, Jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo na baadaye kuzikwa nyumbani Chato Machi 26.
Askofu Bagonza aliyasema hayo jana, katika salamu zake za Noel na heri ya mwaka mpya 2022 alizowatumia waumini wake, akisema mwaka 2021 unaokwisha ulikuwa na habari nyingi mbaya, nyingine za kutisha na zisizoleta furaha.
Sikukuu ya Noel au Krismasi ambayo husherehekewa na waumini wa Kikristo duniani kila inapofika Desemba 25 ni mahsusi kwa siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, wakati mwaka mpya husherehekewa duniani kila inapofika Januari 1.
Habari nyingine ni ugonjwa wa Uviko-19, ukame, mafuriko, uhaba wa maji na kukosekana kwa nishati ya umeme.
Mambo mengine aliyoyataja Askofu huyo ni uvamizi wa magaidi katika mikoa ya kusini mwa Tanzania na majeraha mengi yaliyopo mioyoni mwa watu na kusema kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulitokea katika kipindi cha changamoto zilizopo sasa.
“Hapakuwa na furaha wala matumaini. Taifa teule la Israel lilikuwa chini ya utawala mbaya na watu walikuwa wamekata tamaa. Taifa lisilo na furaha ni mzigo mkubwa kuliongoza,” alisema Askofu Bagonza na kuongeza:
“Furaha ni kitu muhimu sana. Unaweza kuwa na vitu vyote kama fedha, afya, uzao, nafasi, mashamba, kazi nzuri na familia lakini kama hakuna furaha havina maana yoyote. Malaika kuleta furaha kwa watu wote lilikuwa tangazo jema.
“Hata sasa habari njema zinakuja kwetu, lakini baadhi ya habari hizo njema zinakuwa na ubaguzi. Wapo wanaofaidi na wengine kuzikosa. Wateule wachache wanafurahia na wengi wanabaki na shida zao.
“Furaha ya mmoja inakuwa ni huzuni ya mtu mwingine. Lakini kuzaliwa kwa Yesu kulileta habari za furaha kwa watu wote. Ni ajabu! Watu wote tunaalikwa kumpokea Yesu Kristo ili atupatie furaha katika maisha yetu”.
Askofu Bagonza alisema habari hizo njema ni kwa watu wote pasipo ubaguzi na kwamba hizo si habari za kiroho tu, bali hata mwili na akili vinakombolewa na kupata furaha na kusema Yesu haji kuyeyusha shida tu, bali anawapa furaha.
Mwananchi